Novatus asaka historia ya Samata Ulaya

Muktasari:
- Msimu wa 2022/23, Miroshi akiitumikia Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwa mkopo akitokea Zulte Waregem ya Ubelgiji alicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kama ambavyo Samatta alitangulia kucheza michuano hiyo msimu wa 2019-20 akiwa na Genk ya Ubelgiji na hata kufunga bao dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield ambapo timu yake ililala 2-1.
MBWANA Samatta anajiandaa kuandikia historia binafsi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushiriki michuano ya Ulaya zaidi ya mara moja baada ya timu yake ya PAOK FC ya Ugiriki kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuangukia katika Europa League msimu ujao, jambo ambalo Mtanzania mwingine Novatus Miroshi anayekipiga Goztepe ya Uturuki anafukuzia pia.
Msimu wa 2022/23, Miroshi akiitumikia Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwa mkopo akitokea Zulte Waregem ya Ubelgiji alicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kama ambavyo Samatta alitangulia kucheza michuano hiyo msimu wa 2019-20 akiwa na Genk ya Ubelgiji na hata kufunga bao dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield ambapo timu yake ililala 2-1.
Miroshi alicheza mechi yake ya kwanza ya UEFA Champions League dhidi ya FC Porto, chama lake likitandikwa mabao 3-1, mechi ambayo alianza na kumaliza dakika zote 90 na kumfanya aingie kwenye kitabu cha historia ya kuwa Mtanzania wa pili kucheza michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Ulaya.
Msimu huu sasa, timu ya PAOK ya Samatta imeangukia katika michuano ya Europa League na hivyo kujihakikishia kucheza michuano ya Ulaya kwa mara nyingine, na
Miroshi anaitafuta historia hiyo akiwa na Goztepe ambayo inawania kumaliza ndani ya nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi ua Uturuki.
Chama la kiraka huyo liko nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo likiwa na pointi 47 kwenye mechi 33 huku nafasi ya sita ikiwapo Eyupspor yenye nazo 50 ikiwa imecheza mechi 34.
Iko hivi. Mabingwa na washindi wa pili wa ligi wanakata tiketi ya kushiriki katika raundi ya pili ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League).
Timu ya tatu na mshindi wa Kombe la Uturuki (Turkish Cup) wanapata nafasi ya kucheza katika raundi ya pili ya mchujo ya Europa Conference League.
Iwapo mshindi wa Kombe la Uturuki anakuwa tayari amefuzu kwa michuano ya Ulaya kupitia nafasi yake kwenye ligi, basi nafasi hiyo itachukuliwa na timu iliyomaliza katika nafasi ya nne kwenye ligi.
Kila timu inacheza mechi 38 na Goztepe imebakiza mechi tano kujua hatma ya kushiriki michuano hiyo na kutokana na nafasi iliyopo sasa kama itashinda mechi tano zilizosalia inayo nafasi ya kumaliza ndani ya Top 4.
Kama chama hilo litafuzu kucheza michuano ya Ulaya itakuwa ni mara ya pili kwa Novatus kucheza michuano ya Ulaya.