Noela atua Israel, aweka rekodi

Muktasari:
- Noela anakuwa mchezaji wa pili wa kike Mtanzania kusajiliwa na timu inayoshiriki ligi kubwa Ulaya katika dirisha hili baada ya Aisha Masaka aliyetua Brighton inayocheza Ligi Kuu ya Wanawake England.
BEKI wa zamani wa Yanga Princess, Noela Luhala amekamilisha usajili wa kujiunga na Asa Tel Aviv inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Israel kwa mkataba wa mwaka mmoja na kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kusajiliwa na timu inayoshiriki ligi kubwa nchini humo.
Noela anakuwa mchezaji wa pili wa kike Mtanzania kusajiliwa na timu inayoshiriki ligi kubwa Ulaya katika dirisha hili baada ya Aisha Masaka aliyetua Brighton inayocheza Ligi Kuu ya Wanawake England.
Mchezaji huyo ambaye aliachana na Yanga Princess baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu uliopita kabla ya kutua Israel alikuwa akiwindwa na timu mbalimbali chini zikiwemo Fountain Gate Princess na Simba Queens.
Beki huyo wa kati ambaye anaweza pia hucheza beki wa kulia alikuwa ndiye nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya wanawake chini ya umri miaka 17 kilichofuzu na kushiriki Kombe la Dunia India 2022 na kufika robo fainali.
Mwanaspoti linafahamu kwamba Noela alikuwa akiwindwa na timu mbili za Israel, ambapo mbali ya ile aliyojiunga nayo alikuwa akihitajika na Hapoel Tel Aviv.
Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Noela mweye umri wa miaka 18 kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya akiungana na mastaa wengine wa kike ikiwa ni pamoja na Opa Clement na Diana Msewa.
Baada ya kukamilisha dili hilo, Noela anatarajiwa kufunga safari kwenda Israel ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.
Noela ambaye alianza kucheza soka katika timu ya Mapinduzi Queens alijiunga na Yanga Princess 2021 ambako alidumu kwa misimu mitatu kabla ya kuachana nayo mwisho wa msimu uliopita.