Ni zamu ya Messi kutwaa Ballon d’Or
Muktasari:
Ferguson aliongeza kwa kusema Ronaldo ni mchezaji wa kipekee na amekuwa akikomaa kisoka kwa haraka, kiasi hakutarajia katika miaka mitano iliyopita, ndio kwanza ana miaka 23 na bado ana miaka mingi ya maisha yake kutamba katika soka.
Katika toleo lililopita mwandishi Luca Caioli alianza kuchambua mafanikio ya Messi na Ronaldo katika tuzo akichambua tuzo ya kwanza ya Roanldo ya Ballon d’Or ilivyokuwa na jinsi mchezaji huyo alivyowashukuru watu wake wa karibu. Sasa endelea…
“Kama ambavyo kila mtu anafahamu kushinda Ballon d’Or ni kitu ambacho nimekuwa nikikiota tangu nikiwa mdogo na ndio maana hili ni tukio lenye kuvutia na kupendeza kwangu, napenda kuchukua fursa hii kuitoa tuzo hii kwa familia yangu ambayo iko hapa pamoja name,” alisema Ronaldo na kuwageukia wapendwa wake.
“Naitoa kama heshima kwa mama yangu, baba yangu, dada zangu Elma na Katia, kaka yangu Hugo na marafiki zangu wa karibu Rodrigo na Ze pamoja na wakala wangu, Jorge Mendes, ni jambo gumu kuna wengi wa kuwataja lakini ni kwamba nimefurahi sana
Kulikuwa na watu wengi wa kuwashukuru katika hafla ile na zaidi ya hilo pia kulikuwa na mengi ya kushangaza na kufurahisha, kwanza ni video ya Karim Benzema, Samuel Eto’o, Kaka, Luis Figo na wengineo waliompongeza.
Baada ya hapo Sir Alex Ferguson akitoa hotuba yake.
“Ronaldo ana kila sababu ya kupewa tuzo hii na klabu inafurahishwa na mafanikio haya, Manchester United imekuwa ikilisubiri kwa hamu tukio hili kwa miaka 40,’’ alisema Ferguson.
Ferguson aliongeza kwa kusema Ronaldo ni mchezaji wa kipekee na amekuwa akikomaa kisoka kwa haraka, kiasi hakutarajia katika miaka mitano iliyopita, ndio kwanza ana miaka 23 na bado ana miaka mingi ya maisha yake kutamba katika soka.
Hata hivyo, hakuwa Ferguson au mtu mwingine wa karibu aliyefikiri kuhusu Messi ambaye angekuwa akikimbizana kwa kasi na Ronaldo miaka minne ijayo.
Messi ambaye angekuwa wa kwanza kuweka rekodi ya kubeba Ballon d’Or nne mfululizo.
Ballon d’Or ya kwanza aliishinda mwaka 2009 kwa pointi nyingi, alinyakua pointi 473 kati ya 480 zaidi ya mara mbili ya alizopata Ronaldo, aliyekuwa wa pili akipata pointi 233.
Huku akitajwa kuwa wa kwanza kwa miaka 54 ya tuzo hiyo kushinda kwa pointi nyingi namna hiyo.
Pande zote zilikubaliana kwa kuzingatia rekodi za Messi, kiwango chake cha uchezaji, kipaji ubora na namna alivyokuwa profesheno.
“Siwezi kusema uongo, nilijiwa na hisia hilo lingetokea mwaka huu, lakini matokeo ya kura yamenishangaza,’’ alisema akiwa katika mkutano kwenye chumba cha habari cha klabu yake ya Barcelona baada ya kusikia habari hizo.
Ni mchezaji wa kwanza kutoka Argentina kubeba tuzo hiyo na wa kwanza kutwaa tuzo hiyo akiwa ametokea katika akademi ya soka ya Barca maarufu La Masia.
“Tuzo hii ni heshima, na nzuri na ya kipekee lakini sijavimbishwa kichwa na ushindi huu, nilijua kwamba kama ilikuwapo ingetokea tu lakini kwa namna yoyote ile nitaendelea kufanya juhudi vile vile kama kawaida yangu,’’ alisema Messi.
Alipokea tuzo hiyo Desemba 6, katika hafla iliyofanyikia jijini Paris, na kukiri mbele ya hadhara, “Ningependa kushinda hii tuzo kwa mara nyingine, litakuwa jambo tamu na la aina yake kushinda kushinda tena.
Alichokitamani kitokee kikatokee tena mwaka uliofuata ingawa safari hii hakuna aliyetegemea, katika hafla iliyofanyika mjini Zurich, Januari 10, 2011, Messi hakuwa akipewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo hiyo kwa mafanikio yake ya mwaka 2010.
Alikuwa katika orodha iliyokuwa na wachezaji wenzake wa Barca, Andres Iniesta na Xavi Hernandez ambao walitwaa Kombe la Dunia wakiwa na Hispania katika fainali za michuano hiyo mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Kocha Pep Guardiola ndiye aliyefungua bahasha lakini kadi iliyokuwa ndani ilikuwa ikiangalia upande wa watu waliokuwa ukumbini katika hali ambayo haikutarajiwa kila mtu akaona jina na kuibua mshangao kwa hadhara iliyokuwa ukumbini.
Utata ule ulimalizwa baada ya Pep kuigeuza kadi ile kabla ya kutangaza kwa kutaja jina, “Lionel Messi”.
Siku chache baadaye Pep alipoulizwa kuhusu uvumi ulioenea Iniesta ndiyue aliyetabiriwa kuwa mshindi, Pep alijibu kwa kifupi, “Nafikiri Messi ni mchezaji bora.
Akiwa kama aliyechanganyikiwa, kijana mdogo kutoka Rosario aliinuka haraka na kufunga vifungo vya koti lake la suti ya Dolce & Gabbana, akaweka vizuri tai yake shingoni na kutoa kidogo ulimi wake nje kama anavyofanya Michael Jordan anaporuka juu kufunga katika mpira wa kikapu.
Itaendelea Jumamosi ijayo…