Ni Tshabalala ama Mwinyi?
Muktasari:
Vinginevyo timu zote zinapaswa kukubali kushindwa na kumpongeza mshindi t Yanga ya Dar es Salaam na huu ndiyo uungwana (fair play) kama tunavyoona katika nchi zilizoendelea hususan Ligi ya EPL kule England ama La Liga ya Hispania.
LIGI Kuu Bara imemalizika na bingwa pamoja na timu zilizoshuka daraja zimeshafahamika na hakuna mjadala mwingine ila ni kwa timu zilizoshindwa kufikia malengo kukaa chini na kujipanga upya baada ya kujitathimini zilipokosea.
Vinginevyo timu zote zinapaswa kukubali kushindwa na kumpongeza mshindi t Yanga ya Dar es Salaam na huu ndiyo uungwana (fair play) kama tunavyoona katika nchi zilizoendelea hususan Ligi ya EPL kule England ama La Liga ya Hispania.
Ligi hizo zimekuwa zikitazamwa sana na Watanzania tunapaswa kujifunza kuwa ili michezo iendelee lazima uwepo ushindani unaoongozwa na sheria na kanuni na siku zote lazima apatikane mshindi ambaye pia anapaswa kupongezwa.
Tuliona kwa Leiceter City ilipocheza na Cheslea pale Stanford Bridge, wachezaji wa Cheslea walijipanga mstari uwanjani kabla ya mchezo na kuwapongeza kwa kutoa heshima kwa mabingwa wapya kwa kuwapigia makofi ya ukweli na siyo ya kinafiki.
Tukiachana na nasaha hizo ebu tuendelea kuwaangalia wachezaji waliofanya vizuri katika ligi iliyoisha ya 2015-2016. Tayari tumekwisha wazungumzia nyota kadhaa wa nafasi tofauti wanazozicheza uwanjani.
Lengo kubwa la kufanya hivi ni kuendelea kuwahamasisha wachezaji wetu waweze kujituma zaidi ili kulinda na kukuza kiwango wakichagizwa na maoni ya wasomaji juu yao. Utafiti wetu unaonyesha kuwa wachezaji waliong’ara zaidi katika nafasi ya beki wa kushoto (left back) msimu huu kwa maoni ya wengi ni Mohammed Hussein a.k.a Tshabalala wa Simba na Haji Mwinyi wa Yanga, licha ya kuwepo wengine wakali.
Nafasi wanayoitumikia ni maarufu duniani ikibeba kumbukumbu nzito katika historia ya mchezo huu kutokana na umahiri wa nguli kadhaa kuanzia Roberto Carlos beki wa zamani wa Real Madrid na timu ya Brazil enzi zake.
Wapo pia kina Bixente Lizarazu wa Ufaransa iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 1998. Unaweza pia kumzungumzia beki wa Real Madrid Mbrazili, Marcelo anayekimbiza na ukirudi nyuma kidogo pale England unaliona jina la Ashley Cole aliyetamba na klabu za Arsenal na Chelsea.
Tanzania nayo haikuwa nyuma na bado itakumbukwa kwa kuzalisha vipaji hatari vya mabeki wa kushoto, miongoni mwa wachezaji waliosifika ni Mohammed Chuma wa Bandari ya Mtwara, timu ya mkoa huo pamoja na timu ya taifa.
Chuma aliweza kuichezea Taifa Stars kwa nafasi hiyo kwa miaka mingi na kufanya watu waamini kuwa kocha wa timu ya taifa huanza kwa kumchagua beki huyo kisha hufuata wengine hadi alipostaafu mwaka 1975 na kuzawadiwa Radio ya Siera pale Uwanja wa taifa.
Baada ya Chuma kustaafu ndipo yalipojitokeza majina mengi yakavuma vilivyo kama kina Abdallah Msuba wa Cosmopolitan aliyekuwa pia akichezea Kombaini ya Dar es salaam ‘Mzizima United’ katika michuano ya Taifa Cup kabla nafasi hiyo haijaanza kutawaliwa na Mohammed Kajole a.k.a Machela naye akiwa kati ya mabeki bora wa kushoto akiichezea timu ya Simba ya Dar es Salaam.
Kajole atakumbukwa sana kwa aina yake ya uchezaji wa kujituma sana uwanjani akionyesha uzalendo wa kiwango cha juu sana kwa timu yake ya Simba na Taifa Stars; umaarufu wake ulijengeka zaidi kwa uwezo wake wa kupanda na kupiga krosi safi pia upigaji wa mipira ya kona na uchangamfu na mizaha yake kwa wapinzani hali iliyoleta burudani ya aina yake hasa katika mechi za watani wa jadi Simba na Yanga. Kipindi hicho walikuwepo mabeki wengine wazuri sana kina Lucas Nkondola, Tabu Mwakatika (mdogo wake Joram Mwakatika) kule Pamba ya Mwanza na bila kumsahau Mbaraka Mohamed a.k.a Jinga Lao, pia Ally Yusufu wa Yanga waliofuatiwa na kizazi cha kina Ken Mkapa wa Yanga ambaye alifanya kazi ya kutukuka pale Jangwani akiliongoza jahazi kama nahodha aliyedumu muda mrefu. Bado tunawakumbuka kina Douglas Muhani na Said Korongo pale Coastal union, alikuwepo Anwar Awadh pale Yanga wote hawa waliitendea haki nafasi hiyo ya beki wa kushoto.
Nani asiyemkumbuka Yusufu Ismail Bana wa Pamba, Simba na Yanga ya Dar es Salaam, huyu ni miongoni mwa mabeki bora kabisa kuwahi kutokea hapa nchini. Kule Ndovu ya Arusha bado atakumbukwa Simon Kishoka, Mmasai katili uwanjani na beki kisiki ambaye hakuwahi kuwa na masihara kabisa uwanjani wengine waliokuwa bora kweli kweli ni Twaha Hamidu ‘Noriega’ na Alphonce Modest watabaki daima katika kumbukumbu ya soka la Tanzania.
Sasa tuyaangalie mahitaji ya nafasi hiyo kwa mujibu wa majarida ya ufundishaji wa mchezo huu kama inavyosisitizwa katika taaluma ya soka, beki wa pembeni anatakiwa kuwa na uwezo wa kupokonya mipira kwa kuserereka (tackling) zamani ikiitwa laza au yombo.
Pande zote kushoto na kulia, anapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kukaba awe na uwezo mzuri wa kupiga vichwa kutoka pande zote ( all angles) anapaswa kuwa na mahesabu ya uhakika anapokuwa anamkabili adui anayekuja na mpira wa miguu. Anapaswa kuwa mwepesi katika kuingilia kati pasi (interception), anatakiwa kuwa na uwezo wa kutoa pasi fupi na ndefu, pia awe na uwezo wa kupanda kusaidia mashambulizi na awe mwepesi kurudi katika nafasi yake, anatakiwa kuwa mwepesi na fundi mzuri wa soka. Hizi ni baadhi ya sifa zinazohitajika kwa mabeki wa pembeni na wanapozikosa hawapaswi kufikiriwa kupangwa katika nafasi hiyo.
Haya sasa tuwajadili wachezaji hawa wawili ambao kubali usikubali wengi wanaona ndio waliofanya vizuri zaidi katika ligi, Tshabalala na Mwinyi.
Miongoni mwa sifa alizonazo Tshabalala ni uwezo wa kumilliki mpira (ball control) kupandisha mashambulizi, uwezo wa kupiga pasi fupi na ndefu na krosi safi.
Tshabalala pia anao uwezo mzuri wa kunyang’anya mipira, kwa hakika ni beki mzuri kwa wakati huu. Unapomwangalia Mwinyi akiwa kazini uwanjani unafarijika na kupata burudani safi kabisa toka kwa mchezaji huyu mwenyeji wa Zanzibar. Mwinyi anazo sifa lukuki, kwanza kimo chake na nguvu ya mwili, pia ari yake uwanjani. Mchezaji huyu anao uwezo mzuri wa kupandisha mashambulizi, kupiga krosi na ukabaji wake ni wa nguvu na maarifa, kimo chake kinawezesha kucheza vizuri mipira ya juu, ametoa mchango mkubwa sana katika mafanikio ya timu yake msimu huu kabla hajapata matatizo ya kuumia. Udhaifu wa kiufundi ninaouona kwa mabeki hawa wawili ili likiwa ni kosa kubwa ambalo makocha wa timu zao wanaonyesha kutokuligundua kwao ni kukokota mpira kwa zaidi ya sekunde 5 wanapokuwa katika eneo lao la ulinzi.
Taratibu za mabeki zinatoa tahadhari kwa kusisitiza kuwa mabeki wanapoanzisha mpira toka nyuma (build up) wanapaswa kuepuka kukokota mpira (dribbling) kinachotakiwa ni kuanzisha kwa kutumia pasi isipokuwa wanapovuka eneo la katikati ya uwanja kuelekea upande wa timu pinzani ndipo wanaweza kucheza huru kama washambuliaji ingawa kwa tahadhari kubwa.
Ebu tupatieni mawazo yenu ya mpambano wa wiki hii.
Matokeo ya mpambano wiki iliyopita
Kura zilizopigwa – 445
Mwinyi Kazimoto – 215= 49%
Mudathiri Yahaya – 230= 51%
0784-611005