Ngono, tatizo jingine kubwa kwa wachezaji

Muktasari:
- Kumekuwa na hisia kuwa mchezaji wa anaposhiriki tendo hilo la ndoa mara nyingi upo uwezekano mkubwa wa kushusha kiwango chake na hata kupokeza kabisa.
HAKUNA kitu kinachowachanganya wanamichezo wengi kama suala la ngono au tengo la ndoa kwa lugha nyingine.
Kumekuwa na hisia kuwa mchezaji wa anaposhiriki tendo hilo la ndoa mara nyingi upo uwezekano mkubwa wa kushusha kiwango chake na hata kupokeza kabisa.
Huo ndio ukweli wa mambo, ufanywaji wa ngono kwa wachezaji unaweza kumshusha mtu kasi ama la kutegemea na namna atakavyoshiriki. Cheki namna ya kuepuka
ZINGATIA RATIBA
Daktari wa mwenye uzoefu katika kuwatibu wachezaji, Gilbert Kigadye anasema: “Unapofanya tendo la ndoa unatumia nguvu nyingi hivyo usipopata muda wa kurudisha hizo nguvu (kurikava) lazima itakuletea madhara.
“Madhara hayo yatasababishwa na uchovu yaani fatiki ambayo inaweza kuwa chanzo cha kupata maumivu, majeraha na kucheza chini ya kiwango,” anasema Kigadye ambaye pia ni daktari wa Taifa Stars.
Daktari huyo wa zamani wa Azam na Mtibwa Sugar anasema kwa wachezaji ni vizuri wafanye tendo la ndoa wanapokuwa katika kipindi cha mapumziko na wanapokuwa kwenye msimu wa ligi wanacheza mechi na kufanya mazoezi magumu, waifanye kwa uchache huku wakiangalia muda kama wana mchezo karibu au hawana.
Daktari wa Azam, Mwanandi Mwankemwa amesema, “Watu wanatakiwa kufahamu kuwa, tendo la ndoa au ngono kama linavyoeleweka ni la kawaida kwa kila binadamu lakini analifanya katika mazingira yapi ndiyo kitu cha kuzingatia.
“Kitu cha kwanza, ngono kwa wachezaji inaondoa msongo wa mawazo ‘stresi’ au ‘tensheni’ ya mambo mengi hasa kwenye ushindi wa timu husika,” anaeleza Mwankemwa na kutolea mfano kwa wale wanaovuta bangi, wengi wao wanaishiriki kwa ajili ya vitu kama hivyo, kuondoa msongo wa mawazo na kumjengea ujasiri lakini kumbe kitu kile huwa ni cha muda na baadaye kinaumiza.
“Kuna wakati timu inakabiliwa na mechi ngumu jambo linalowafanya mchezaji kujenga hali ya woga, lakini anaposhiriki ngono inaweza kumwondolea mchezaji huyo hali hiyo na kumjenga akawa katika hali ya utayari kupambana,” anaeleza Mwankemwa ambaye anatajwa kuwa mmoja kati ya madaktari wa michezo nchini wenye sifa na vigezo.
Mwankemwa ametolea mfano katika michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2014 pale kocha wa Brazil Felipe Scolari alipowaruhusu wachezaji wake kushiriki ngono na hata katika mechi yao dhidi ya Italia, ambayo walishinda.
Anasema, Scolari aliwaona wachezaji wake hawako fiti na wanakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Italia na mbinu aliyotumia ilikuwa ni kuwaruhusu wachezaji kufanya yao.
KUJITAMBUA TU
Kocha wa KMC , Felix Minziro maarufu kwa jina la Baba Isaya anasema: “Kwa mchezaji anayefanya ngono inaweza kumuathiri pale tu anapokuwa hana mpangilio maalumu si unaona wachezaji wanaoa.
“Kinachatakiwa mchezaji anapaswa kujitambua anatakiwa kufanya kwa wakati gani eti unaona Jumapili una mechi Jumamosi unafanya ngono lazima itakusumbua. Na hii kwa upande wetu sisi Waafrika ndiyo inatusumbua lakini kwa wenzetu Ulaya wanajua namna ya kufanya ndiyo maana unaona hawaingii hata kambini,” anafafanua Minziro kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga.
UGALI UNASAIDIA
Beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Oscar Joshua anasema: “Ngono hata kwa misingi ya dini imeruhusiwa lakini ina miiko yake, iko hivyo hata katika mpira. Binafsi nilikuwa nafanya lakini nilikuwa naangalia ni kwa wakati gani na baada ya hapo nifanye nini. Siku tatu kabla ya mechi sikuwahi kufanya na nilikuwa nafanya hivyo mara tu tunapomaliza mechi, tukiruhusiwa kwenda kwenda kupumzika.”
“Hata hivyo baada ya mechi nilikuwa naangalia kama mechi zinakuwa zimefuatana, huwa naachana nayo kwa sababu najua itaniletea madhara, pia ninapofanya hivyo najitahidi kula vyakula vya kujenga mwingi na kuupa nguvu mwili kama ugali, hii ilinisaidia,” anaeleza Oscar ambaye kwa sasa amesimama kucheza soka na anafanya shughuli nyingine.
UKITHUBUTU UMELIWA
“Kama unavyojua kitu chochote unapokishiriki kwa wingi kinaumiza na ndivyo ilivyo katika ngono, unachotakiwa ni kutambua unaifanya katika wakati gani na kwa namna gani. Unaweza kuwa na mechi karibu wewe unajiendekeza, utakwisha,” anasema Mwankemwa na kufafanua hiyo huwa inawaathiri zaidi wachezaji wa Kiafrika ndiyo maana kumekuwa na tabia ya kukaa kambini, lakini kwa wachezaji wanaojielewa kama Ulaya hakuna mambo hayo kwa sababu anakuwa anajua wakati gani wa ngono na aifanye vipi.
“Unaposhiriki ngono bila mpangilio iko wazi utapoteza nguvu nyingi na kama unavyojua mazoezi ya mpira au mechi inahitaji nguvu nyingi hivyo utakaposhiriki tendo hilo kwa nguvu halafu unakwenda kucheza mechi au mazoezi hutacheza kwa kiwango.
Daktari huyo ambaye kwa sasa anawatibu wachezaji wa Azam FC anatoa onyo pia kwa wale wachezaji wanaopenda kuufanya mchezo huo mara kwa mara kuwa ni tatizo kwani utakapokwenda mazoezini au kwenye mechi utakuwa mtu wa kuchoka kila siku kushindwa kufanya mazoezi kwa ustadi na ikiendelea hivyo basi unakuwa unajiua kiwango.
“Lakini, unapoifanya kwa mpangilio kwa kujipa muda wa kutosha wa mapumziko, kucheza mechi na wa mazoezi, ngono haiwezi kuwa tatizo kwako,” anaeleza.
VIPI UKIWA MAJERUHI?
Mwankemwa anafafanua kwa wale wachezaji wanaoshiriki tendo hilo wakati ni wagonjwa au majeruhi kwa kuanika kwamba; “Kwa mchezaji mwenye kuumwa, maumivu au majeraha ya kawaida tendo la ndoa linamsaidia kisaikolojia na kumfariji lakini alifanye kwa ungalifu, inaweza kuwa tatizo kwa yule aliyevunjika goti, enka kama hatakuwa makini katika ufanyaji tendo hilo, anaweza kujitonyesha na kuibua tatizo upya ambayo yatamuweka nje kwa muda mrefu ama yanaweza kumafanya ashuke kiwango.