Nabi apewa mechi mbili, mwenyewe ajitetea

MATOKEO ya juzi dhidi ya Rivers United hayajawafurahisha mabosi wa Yanga na kulazimika kufanya vikao vya kimyakimya kuona namna gani watapenya mechi ya marudiano huko Nigeria Jumapili hii na wataikabili vipi Simba Septemba 25.

Yanga ilifungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, matokeo ambayo yamewavuruga vigogo ambao sasa wanaumiza vichwa wakitafakari mechi hizo mbili ambazo zinaonekana kubeba hatima ya kocha Nasreddine Nabi.

Mechi hizi mbili pamoja na ile ya Simba zinatajwa kuwa zitaamua ajira ya Nabi.Sababu mbalimbali zimetajwa kumuweka katika wakati mgumu na huenda lolote likamkuta ingawa viongozi wanalisema hilo chinichini. Sababu mojawapo inatajwa kuwa ni kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya wasaidizi wake ikiwemo wale walioondoka hivikaribuni klabuni hapo. Inadaiwa kuwa wasaidizi hao walikuwa wakimshauri lakini hakuwa akizingatia na kama haitoshi aliwaambia viongozi anataka wasaidizi wengine ambao walikuwa raia wa Tunisia waliokwenda hadi Morocco, lakini walizuiwa uwanja wa ndege na kushindwa kujiunga kambini na wakajiunga na timu Dar.

Hata waliporejea nchini aina ya mazoezi ambayo wamekuwa wakifanya na muda wanaotumia wachezaji wamekuwa wakiyalalamikia chinichini.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa mabosi hawakufurahishwa pia na kikosi kilichopangwa wakati wa mechi hiyo hata aina ya mabadiliko ya wachezaji aliyoyafanya wakati mchezo unaendelea. Habari zinasema kuwa ishu ya kumtomchezesha Bangala na kumpa Saido dakika chache kimewakera viongozi wa Yanga. Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imedokezwa na mmoja wa vigogo wa Yanga ni kwamba kama watashindwa kuivuka Rivers na ile ya Septemba 25 dhidi ya Simba, Nabi anaweza kuonyeshwa mlango na nafasi yake ikashikiliwa kwa muda na Mwinyi Zahera ambaye wiki hii atatambulishwa kama Mkurugenzi wa Ufundi wa soka la vijana, lakini uongozi utashauri amsaidie Nabi kwenye mechi ya ugenini. Alipotafutwa Nabi alisema kushindwa kupata muda wa kutosha kufanya maandalizi akiwa na wachezaji wote Morocco na hata hapa nchini ndio kumechangia matokeo mabovu.

“Jambo hili si salama kabisa, lakini haina jinsi, tunarudi katika mazoezi kuandaa timu kwa ajili ya mchezo wa marudiano na kuona aina gani ya matokeo tutayapata ugenini,” alisema Nabi.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema Yanga ilikuwa lazima wapate wakati mgumu kucheza na Rivers kwani hawakuwa pamoja wachezaji wote kufanya maandalizi kama ilivyokuwa wapinzani wao. “Kutokana na kiwango ambacho Yanga walikionyesha mechi ya kwanza sioni kama wanaweza kupindua matokeo ugenini kutokana maandalizi yao ambayo wameyafanya, sio imara ingawa katika soka lolote linaweza kutokea,” alisema.


KUWAFUATA RIVERS

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa vigogo wa timu hiyo wametangulia nchini Nigeria wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa aliyeenda kuandaa mazingira ya kufikia na kuangalia namna gani wanaweza kupindua matokeo kibabe na kuzima fitna za Wanigeria hao.

Yanga haijatoa taarifa rasmi kwa uongozi wa soka Nigeria lini itatua nchini humo na imepanga kuwasapraizi ili kukwepa mitego ya wapinzani wao na tayari imekamilisha taratibu zote za kuondoka na ndege ya kukodi ambayo itakuwa na watu wa Yanga pekee.

Moja ya vigogo wa timu hiyo, ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Mashabiki wetu wawe na subra kwani bado nafasi tunayo na naamini tutaenda kushinda kwao kama wao walivyoshinda kwetu.”