Nabi ana dawa ya Okrah, matajiri Yanga watua kambini

YANGA ikiwa na sura nyingi mpya, imefanya kikao na mastaa wao chini ya kocha Nasreddine Nabi ambaye ametamka kwamba; “Wamenielewa.”

Nabi katika kikao hicho kilichotumia dakika 15 amewakumbusha wachezaji wake kwamba katika mchezo wa kilele cha Wiki ya Mwananchi, waliwazingua mashabiki na viongozi wao baada ya kufungwa na Vipers ya Uganda.

Hata hivyo Nabi amewaambia wachezaji wake waachane na matokeo hayo ingawa wanatakiwa kutambua kwamba matokeo hayo yamewapa shida mashabiki wao mitaani na sasa leo Agosti 13 wakabadili huzuni hiyo kuwa furaha.

Baada ya kikao hicho juzi hiyo likapigwa tizi kali na kila staa akionyesha yuko katika hali ya kuhitaji pambano hilo la ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu Bara msimu wa 2022/23.

Mbali na akili hiyo ya Nabi pia kocha huyo akafichua anawajua mastaa wote wapya wa Simba kasoro Mserbia tu Dejan Georgijevic na kwamba anajua mazuri na mapungufu yao ambayo ameongea na wachezaji wake.

Nabi alisema alipofanya kazi El Merrikh ya Sudan anafahamu taarifa za kutosha juu ya kiungo mshambuliaji mpya wa Simba Augustine Okrah na kwamba anajua jinsi ya kumdhibiti.

“Namjua Okrah vizuri sana wala sio mchezaji ambaye kwangu ananishtua nina marafiki pia bado wapo Sudan ambao wanamjua vizuri, hata yule Okwa (Nelson) tulishakutana naye ni mchezaji kama Okrah nafahamu ubora wake tangu tulipokutana naye.

Ouattara (Mohamed) ni beki mzuri lakini najua ubora upi wachezaji wangu wawe nao ili waweze kupenya ukuta wangu labda yule raia wa Serbia (Dejan) sijamjua vizuri lakini nafahamu timu yangu iwe vipio kuhakikisha tunatoka salama na ushindi.

“Nafurahi kuona morali ya wachezaji ipo juu sana na wanapambana sana mazoezini, kila mchezaji anajua ni jinsi gani tuliwapunguzia furaha mashabiki wetu katika mchezo wa Jumamosi iliyopita na sasa wafanye kipi.”

Matajiri Yanga

watua kambini

Mabosi wa Yanga ambao wameteuliwa Jumatano katika Kamati ya Mashindano baada ya kufanya kikao chao juzi ikiwa ni siku ya kwanza tangu wateuliwe na Rais wa klabu hiyo injinia Hersi Said jana walitua kambini kuongea na wachezaji kwa ajili ya kuwapa mzuka.

Hata hivyo, hakuna aliyejua kilichozungumzwa baina ya mabosi hao na wachezaji hao, lakini inaelezwa lengo lilikuwa kuwahamasisha ili kuendeleza raha kwa mashabiki wa klabu hiyo kama ilivyotokea msimu uliopita walipoifumua Simba kwa bao 1-0 kwenye mechi kama hiyo ya Ngao. Baada ya ile ya Vipers waliyopoteza hii ndiyo itakuwa mechi ya pili ngumu ya Yanga msimu huu kwani wamecheza mechi nyingi na timu za madaraja ya chini.