Mzungu wa Yanga ajiuzulu Yemen
MWANDISHI WETU KOCHA wa zamani wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amejiuzulu kuifundisha timu ya Taifa ya Yemen Jumamosi iliyopita kutokana na matokeo mabovu pamoja na mazingira magumu ya kazi. Tom aliondoka Yanga Oktoba mwaka jana baada ya kutofautiana na uongozi wa juu sababu kubwa ikielezwa kuwa ni mdomo wake, matokeo mabovu ya mechi za kwanza za ligi pamoja na kutotaka kuburuzwa. Kocha huyo alithibitisha kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba ameacha kazi na akatuma barua pepe Shirika la Habari la Reuters Jumamosi kwamba amebwaga manyanga ingawa hakueleza sababu. "Nawashukuru wachezaji na viongozi kwa ushirikiano pamoja na watu wa Yemen, ni nchi nzuri na nitaikumbuka daima kwa vile iko kwenye moyo wangu,"alisema kocha huyo maneno ya kujikosha ambayo aliyatoa pia wakati anaondoka Yanga. Habari za ndani kutoka kwenye magazeti ya Yemen ni kwamba kocha huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili Oktoba amekimbia kutokana na matokeo mabovu kwani katika mechi zisizopungua sita akiwa kwenye benchi hawajashinda hata moja. Timu yake ilitolewa mapema kwenye harakati za kuwania Kombe la Dunia na Iraq na hata kwenye michuano ya Kombe la Asia wanashikilia mkia kwenye kundi. Wamecheza mechi mbili za Kundi D dhidi ya Bahrain (nyumbani) na Malaysia (ugenini) na kupoteza zote huku ikiwa imesaliwa na mechi nyingine nne ambazo inadaiwa hakuona dalili ya ushindi ndio maana akaingia mitini mwenyewe. Wachambuzi wa soka wanadai pia kuwa hata kitendo cha mamlaka za soka kuhamishia mechi za nyumbani za Yemen Falme za Kiarabu kutokana na sababu za usalama pia kimechangia kumkatisha tamaa Tom ambaye kitabia ni mtu mkali na asiyependa kupindisha maneno.