Mzamiru ajifunga miaka miwili TRA United
Muktasari:
- Kwa mara ya kwanza kiungo huyo alijiunga na klabu ya Simba msimu wa 2016-2017 akitokea Mtibwa Sugar na msimu uliyoisha Wanamsimbazi hao walimtoa kwa mkopo kwenda TRA United.
BAADA ya kiungo mkabaji Mzamiru Yassin kumaliza mkataba wa mkopo wa miezi sita aliyokuwa akiuchezea TRA United kutoka Simba, imeelezwa ameanza safari yake mpya nje na Wanamsimbazi hao.
Kwa mara ya kwanza kiungo huyo alijiunga na klabu ya Simba msimu wa 2016-2017 akitokea Mtibwa Sugar na msimu uliyoisha Wanamsimbazi hao walimtoa kwa mkopo kwenda TRA United.
Chanzo cha taarifa kutoka kwa mtu wa karibu na kiungo huyo, zilisema baada ya Mzamiru kumaliza mkataba wake wa mkopo na Simba haikutaka kufanya naye mazungumzo mapya, hivyo aliamua kuendelea na maisha yake mapya nje na klabu hiyo.
Chanzo hicho kilisema:"Mzamiru tayari ameishasaini mkataba wa miaka miwili na TRA United ambayo imeona huduma yake inahitajika kwa ajili ya msimu ujao," kilisema chanzo hicho na kuongeza;
"Simba ilimtoa kwa mkopo ili kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara, lakini naona kocha Steven Barker ameona hahitaji kuendelea naye tena na tayari Yusuf Kagoma kiwango chake kimewaka."
Chanzo hicho kilisema Mzamiru kabla ya kusaini mkataba huo na TRA kuna timu zilikuwa zikitaka huduma yake kama Namungo FC, JKT Tanzania na Pamba lakini aliona bora aendelee kusalia hapo.
"Aliona bora aendelee kusalia katika timu ambayo tayari alishaanza kupata nafasi na ina ushindani mkali wa namba unaompa chalenji ya kujituma kwa bidii," kilisema chanzo.
Mzamiru akiwa na Simba alivaa medali za ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo msimu wa 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21, hivyo anaachana na timu akiwa amejenga CV kubwa kwa sasa Shomary Kapombe pekee ndiye mchezaji aliyedumu kwenye timu hiyo kwa muda mrefu akiwa alijunga na timu hiyo mwaka 2017.