Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muziki mpya wa Yanga noma

Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi

Muktasari:

Kocha huyu mpya raia wa Uholanzi alianza mazoezi juzi Jumamosi, si muumini wa soka la kujilinda bila kushambulia na anapenda kazi ya kuzuia ifanywe na kila mchezaji wake kikosini bila kujali nafasi achezayo.

KWA mtazamo wa haraka katika programu za kwanza za mazoezi ya kocha mpya wa Yanga,Hans van der Pluijm ni kwamba kutatokea mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza.

Kocha huyu mpya raia wa Uholanzi alianza mazoezi juzi Jumamosi, si muumini wa soka la kujilinda bila kushambulia na anapenda kazi ya kuzuia ifanywe na kila mchezaji wake kikosini bila kujali nafasi achezayo.

Hii ni mara ya pili kwa Pluijm kupewa jukumu la kuifundisha Yanga baada ya awali kupewa kazi hiyo akichukua mikoba ya Ernie Brandts ambaye aliachishwa kazi na timu hiyo baada ya kupoteza mchezo wa Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba mwaka jana.

Kabla ya ujio wake, Yanga ikiwa chini ya Kocha Marcio Maximo imekuwa ikicheza soka la kujilinda na kujikuta ikitengeneza nafasi chache za kufunga, na hata ikipata ushindi huwa wa mabao kiduchu. Yafuatayo ni mabadiliko yatakayofanywa na Pluijm katika kusuka muziki mpya wa Yanga;

Mbuyu Twite arudi kulia

Kwa sasa Mbuyu Twite anacheza kiungo mkabaji lakini wakati wa Pluijm alikuwa anacheza beki ya kulia ambapo alikuwa anacheza huku akipandisha mashambulizi ya timu yake na kuzuia wakati huohuo. Huko Twite huwajibika ipasavyo katika kuzuia mashambulizi ya mawinga wasumbufu kama Emmanuel Okwi na Deus Kaseke wa Mbeya City. Beki wa sasa wa kulia wa Yanga, Juma Abdul hataweza kuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha sasa kwani kitendo chake cha kupandisha timu na kuchelewa kurudi katika nafasi yake kitamgharimu na anatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha anarudisha imani kwa kocha wake. Ikitokea Twite akiwa majeruhi au vinginevyo basi Salum Telela atacheza beki ya kulia kwani ana uwezo wa kuzuia na kupandisha timu.

Hassan Dilunga kurudi kikosini

Hadi katika mechi ya mwisho ya Maximo dhidi ya Simba, kiungo Hassan Dilunga alikuwa benchi kwani hakuendana na mfumo wake wa kuzuia kwa muda wote bila kuipeleka mbele timu. Maximo alitoa nafasi kwa Twite na Emerson Roque kucheza nafasi hiyo lakini alilazimika kumuingiza Dilunga dakika ya 45 baada ya Twite kuumia. Pluijm hata kabla hajaondoka alikuwa anamuamini kuwa kiungo mzuri na alimtumia katika mechi kadhaa akicheza kwa kuzuia na kushambulia japokuwa si mzuri sana kwenye kuzuia. Taratibu Dilunga atarejea kikosini lakini kiungo Said Juma ‘Makapu’ ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuanza kwani ni mzuri katika kuzuia na kupandisha timu na tayari Pluijm anamuandaa ili achezea dhidi ya Azam FC Desemba 28, mwaka huu. Makapu alifanya vizuri katika mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Azam ambayo Yanga ilishinda mabao 3-0 na kocha ameshapewa taarifa hizo hivyo anapanga kumrejesha katika nafasi hiyo huku msaidizi wake akiwa Dilunga. Hivyo, Makapu ataanza na kama mambo hayataenda vizuri basi Dilunga ataingia kuchukua nafasi yake ili kuokoa jahazi. Maximo hakuendelea kumpa nafasi Makapu licha ya kucheza vizuri dhidi ya Azam.

Kaseja benchi

Ingawa bado anavutana na viongozi wa Yanga, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kipa Juma Kaseja kuanza mazoezi ya kuichezea Yanga na kurejeshwa moja kwa moja katika kikosi cha timu hiyo akimsaidia kipa namba moja Deo Munishi ‘Dida’ kwani tangu zamani Pluijm alimfanya Kaseja kuwa msaidizi wa Dida. Hii inamaanisha kwamba, Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye sasa ni namba mbili huenda akalikumbuka dirisha dogo kwani ataondoka benchi na kusubiri jukwaani endapo Kaseja atakuwa katika ubora wake. Pluijm anapanga kumrudisha Kaseja uwanjani licha ya kipa huyo kutotokea katika mazoezi ya Yanga tangu ligi iliposimama na hakushiriki maandalizi ya mechi ya Nani Mtaji Jembe.

Salum Telela katikati

Kiungo Salum Telela anaweza kuwa mmoja wa wachezaji wa Yanga wanaofurahia kurejea kwa Pluijm kwani ni kipenzi cha kocha huyo raia wa Uholanzi. Pluijm anapanga kumchezesha Telela kiungo namba sita na kama ikitokea mambo yakiharibika kwa Twite basi kiungo huyu atacheza namba mbili yaani beki wa kulia kwani anamudu kucheza nafasi hiyo. Kwa sasa Telela anaonekana yupo fiti baada ya kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu hivyo kuwa mtu wa benchi japokuwa ana uwezo mkubwa wa kucheza soka. Hata hivyo kwa sasa ataanza Makapu kutokana na uwezo wake kuonekana kumvutia kocha kutokana na kufanya vizuri dhidi ya Azam katika mechi ya Ngao ya Hisani.

Hussein Javu kung’ara

Yanga sasa ina mastraika wanne ambao ni Kpah Sherman, Danny Mrwanda, Amissi Tambwe na Hussein Javu. Kati ya hayo kocha amepanga kuwaanzisha Sherman na Tambwe huku Mrwanda akisikilizia lakini Javu ndiye ‘Super Sub’ wake hata mchezaji mwenyewe anafahamu hilo. Sherman ni uhakika kikosi cha kwanza lakini Tambwe na Mrwanda watakuwa wakipokezana kulingana na mechi ilivyo, lakini Javu ndiye Super Sub wao. Pluijm ana imani na Javu kwani anajua ni mchezaji anayetumia akili sana wakati wa kushambulia. Javu anaweza kuwa katika nafasi ya kucheza zaidi kwa sasa kwani Pluijm amepanga kumchezesha Mrwanda katika winga ya kulia lakini akibadilishana na Simon Msuva kulingana na timu watakayocheza nayo, hivyo atapunguza hali ya kunyang’anyana namba nafasi ya ushambuliaji wa kati wakati Tambwe na Sherman wakianza.

Matumizi ya mastraika wawili

Kwa sasa Yanga inacheza kwa kutumia mshambuliaji mmoja tu, lakini kutokana na aina ya wachezaji iliyonayo timu hii sasa itacheza kwa kuwatumia washambuliaji wawili ambao ni Sherman na Tambwe ili kutafuta ushindi wa mabao mengi mapema na kuondokana na soka la mipira mirefu ambalo limeonekana haliwezi kuisaidia timu hiyo.

Yanga mpya

Kutokana na mabadiliko hayo pamoja na mtazamo na mazoezi ya Pluijm, Yanga mpya ni wazi kwamba itapangwa hivi; Dida, Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Danny Mrwanda, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Kpah Sherman, Simon Msuva.