Moto Chini

Muktasari:
- Wakati baadhi ya mastaa kama Haruna Niyonzima na Ibrahim Ajibu wakishindwa kufanya makubwa kwenye timu walizokwenda, nyota hao wametikisha kinoma. Kwanza unaambiwa hawakosekani kwenye vikosi vya kwanza.
KATIKA Msimu uliopita wa Ligi Kuu tulishuhudia baadhi ya wachezaji wakitesa na timu fulani na mwisho wa msimu wakapata malisho mapya. Sasa unaambiwa huko walikokwenda wanawasha moto hatari.
Wakati baadhi ya mastaa kama Haruna Niyonzima na Ibrahim Ajibu wakishindwa kufanya makubwa kwenye timu walizokwenda, nyota hao wametikisha kinoma. Kwanza unaambiwa hawakosekani kwenye vikosi vya kwanza.
Pili ni kwamba wamekuwa na kiwango cha kuvutia katika kila mchezo jambo ambalo limewafanya waonekane mashujaa wakubwa wa timu hizo. Unafahamu ni kina nani?
Mwanaspoti inakuletea orodha ya baadhi ya Wachezaji ambao waling’aa na timu zao msimu huo, lakini hata waliposajiliwa kwenye timu nyingine msimu huu hadi sasa bado wamekuwa na kiwango Bora.
SAimon Msuva
(Difaa El Jadida)
Winga huyu wa zamani wa Klabu ya Yanga, anayekipiga nchini Moroco katika Klabu ya Difaa El Jadida, bado nyota yake inazidi kunga’aa kwani tayari ameifungia timu yake mabao 10 na kuwa kinara wa mabao kwa wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu nchini humo.
Wakati nyota huyo akiwa Jangwani aling’aa na kuwa ‘Lulu’ kwani aliipa mafanikio makubwa Klabu hiyo ikiwamo Ubingwa mara tatu mfululizo.
Pia katika msimu wake wa mwisho alikuwa mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara sambamba na Abdulrahaman Mussa wa Ruvu Shooting baada ya kufunga mabao 14 kila mmoja.
Msuva amewahi pia kuwa mchezaji bora pamoja na mfungaji bora wa Ligi Kuu mwaka 2015, hivyo kuwa miongoni mwa wachezaji wa viwango vya juu nchini.
Huko Morocco unaambiwa amekuwa Mfalme na timu yake ya Difaa El Jadida inamtegemea katika kufunga na kutengeneza mabao.
Abdi Banda (Baroka)
Kiraka wa zamani wa Simba, Abdi Banda naye anauwasha moto huko Afrika Kusini kinoma.
Banda alijiunga na Baroka FC ya Afrika Kusini mara tu Ligi Kuu ilipomalizika, na amekuwa mchezaji muhimu katika timu hiyo akipangwa karibu mechi zote.
Kabla ya kutua Sauzi, Banda alikuwa mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Simba, akipangwa kama beki wa kati ama kiungo, nafasi ambazo alicheza kwa ufanisi mkubwa.
Aishi Manula (Simba)
Kipa huyu wakati anaitumikia Azam alikuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kuipa ubingwa Ligi Kuu msimu wa 2013/14, huku akiwa na uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza.
Akiwa Azam alishinda pia mataji mawili ya kombe la Mapinduzi na moja la Kagame, hivyo kuwa miongoni mwa wachezaji wenye mafanikio makubwa nchini.
Manula alishinda pia tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo mwaka 2016 na 2017 kabla ya kuihama Azam FC na kutua Simba.
Katika kikois cha Simba ameendelea kuwa wa moto kwani amekuwa ni chaguo la kwanza tangu kuanza kwa msimu mpaka sasa tena akicheza kwa kiwango cha juu.
Pius Buswita (Yanga)
Mshambuliaji huyu chipukizi ameendelea kuwa mtamu tangu akiwa Mbao FC, ambapo hadi sasa ana uhakika wa namba kwenye timu yake mpya ya Yanga.
Licha ya ushindani uliopo Klabuni humo, bado nyota huyo ameweza kulishawishi benchi la ufundi la Bingwa huyo mtetezi kucheza kikosi cha kwanza na kwa mafanikio.
Buswita ambaye alikuwa nyota tegemeo kwenye timu ya Mbao ya Jijini Mwanza ni msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu, lakini amefanikiwa kung’ara katika timu zote mbili alizocheza.
Asante Kwasi (Simba)
Hakuna ubishi kuwa Kiraka huyu raia wa Ghana amekuwa bora tangu alipotua nchini mwaka juzi na kujiunga na Mbao FC.
Kwasi ni miongoni mwa wachezaji walioipa jina kubwa Mbao FC katika msimu wake wa kwanza. Akiwa nahodha, aliiongoza timu hiyo kufika fainali ya kombe la FA, rekodi ambayo itakumbukwa miaka nenda rudi.
Kwasi tangu atue hapa nchini,amekuwa ni mchezaji mwenye rekodi nzuri katika kazi yake ya mpira na hapa wengi wanaweza kukubali alipokuwa na Mbao FC kisha Lipuli aliyoichezea katika duru la kwanza msimu huu.
Adam Salamba (Lipuli)
Straika huyu ambaye mwezi Machi alichaguliwa Mchezji Bora wa Ligi Kuu, ni kama tu anafanya mwendelezo wa rekodi nzuri katika Soka, kwani hata alipokuwa Stand United kazi yake ilikuwa tamu kinoma.
Hadi sasa nyota huyo amekuwa tegemeo kubwa kwenye kikosi cha Lipuli kwani tayari ameifungia mabao manane na kufikia hatua ya kutamaniwa na klabu vya Simba na Yanga.
Uwezo wake wa kujituma uwanjani na kutokata tamaa imemfanya chipukizi huyu kuwa mtamu kila kona na huenda hata msimu ujao akavaa uzi wa Njano au Mwekundu.
Awesu Awesu (Mwadui)
Kiungo huyu kazi yake ilianza kuonekana akiwa na timu ya Madini FC ya mkoani Arusha inayoshiriki Ligi Daraja la Pili. Alipata umaarufu mkubwa zaidi alipowatoa jasho mastaa wa Simba katika robo fainali ya kombe la FA mwaka jana.
Licha ya Simba kushinda bao 1-0, walikumbana na kasheshe ya kiungo huyo mwenye rasta.
Moto aliouonyesha Uwesu,bado ni uleule kwenye timu yake ya Mwadui na ni wazi Simba wanammezea mate hadi sasa kutaka akakipige huko.
John Bocco (Simba)
Straika huyu mtata nchini hakuna asiyejua uwezo wake tangu alipokuwa Azam. Bocco ameshinda mataji manne ya Mapinduzi, moja la Kagame na moja la Ligi Kuu katika kipindi cha miaka tisa aliyoichezea Azam FC.
Msimu huu alijiunga na Simba ambako amekuwa lulu pia. Bocco ndiye silaha kubwa kwa sasa Simba na ameweza kuifungia mabao 14 huku akipika mengine kadhaa.
Wakati alipotua Msimbazi, wapo waliobeza kuwa ni mzee na hawezi kufurukuta, lakini anachofanya hivi sasa kila mmoja ni shahidi.
Shomari Kapombe (Azam/Simba)
Alisajiliwa na Simba msimu huu ambapo mechi za mwanzo hakucheza kutokana na kusumbuliwa na majeraha jambo ambalo lilifanya wengi kubeza usajili wake.
Kapombe alisajiliwa na Simba akitokea Azam FC ambapo nako alidumu kwenye kikosi cha kwanza kwa muda mrefu huku akicheza kwa kiwango cha juu.
Lakini baada ya kurejea uwanjani ameonyesha kiwango kikubwa jambo ambalo limefanya sasa kuweza kuwepo kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Pierre Lechantre.
Kapombe alikuwa majeruhi lakini alipopona amekuwa kama hakuwa majeruhi anavyoupiga.