Azam: Tunajua namna ya kuwakabili Yanga
Muktasari:
- Kauli hiyo ameitoa wakati kesho Juni 24, 2026 timu hizo zinakwenda kukutana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja kuanzia saa 10:00 jioni.
KOCHA Msaidizi wa Azam, Kassim Liogope, amesema kitendo cha kukutana na Yanga kwa mara tano ndani ya msimu mmoja, kwao inawapa picha halisi ya mpinzani gani wanakwenda kukabiliana naye, hivyo wapo tayari kwa ushindani.
Kauli hiyo ameitoa wakati kesho Juni 24, 2026 timu hizo zinakwenda kukutana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja kuanzia saa 10:00 jioni.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara, ni muhimu kwa timu zote kushinda kwani Yanga inahitaji kuendelea kukaa kileleni ili kutengeneza njia ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo ikiwa na pointi 66, wakati Azam ikisaka heshima na nafasi bora zaidi kwenye msimamo ikikusanya pointi 58 ikikamata nafasi ya tatu. Katikati yao kuna Simba yenye pointi 64.
Akizungumzia mchezo huo, Liogope amesema: "Mchezo wetu wa kesho dhidi ya Yanga tumejipanga vizuri na tunajua utakuwa mchezo mgumu kutokana na timu zote mbili na kikubwa mwaka huu tunakutana zaidi ya mara nne. Kwa hiyo tunamjua mpinzani tunayecheza naye ni wa aina gani.
"Yanga ni timu nzuri na ina wachezaji wengi wazoefu, pia mwalimu mzuri, kwa hiyo ni aina ya mechi ambayo itakuwa na ushindani.
"Lakini sisi kama Azam ni aina ya mechi ambazo tunazipenda kwa sababu ni mechi ambayo inakuwa ya ushindani. Lakini kitu kikubwa najua tulicheza nao kama siku mbili zilizopita, muda tulioupata wa maandalizi tumeangalia sehemu zenye upungufu na kuzifanyia kazi kuhakikisha kesho tunaingia kamili lengo ni kushinda."
Wakati huohuo, nahodha na beki wa kulia wa Azam, Lusajo Mwaikenda, amesema: "Ninaamini Yanga ina kikosi kizuri kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa katika ligi yetu. Na sisi kama wachezaji wa Azam tutajiandaa kucheza na timu nzuri.
"Hakuna mchezaji mmoja wa kumuangalia, mechi itakuwa ya ufundi mwingi na sisi tupo tayari kuwakabili wapinzani wetu."
Rekodi zinaonesha kwamba, Yanga na Azam zimekutana mara 35 katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 2008 ambapo Yanga imeshinda mechi 14, Azam ikishinda 11, sare zikiwa 10. Katika rekodi hizo, yamefungwa mabao 89, Yanga inayo 46 na Azam 43.
Timu hizo zinakutana baada ya siku tatu kupita ambapo mara ya mwisho ilikuwa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB iliyochezwa Juni 21, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Azam kushinda mabao 3-2.
Pia msimu huu itakuwa mara ya tano timu hizo zinakutana baada ya kuanza kwa matokeo ya 0-0 Ligi Kuu Bara, kisha Yanga kushinda kwa penalti 5-4 kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, pia Yanga ikashinda tena 2-1 katika nusu fainali ya Kombe la Muungano, Azam ikajibu mapigo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa mabao 3-2.