Mmeona lakini! Simba kuhamia kambi ya ushindi Dar

Tuesday April 26 2022
Simba PIC
By Ramadhan Elias

SIMMEONA! Ndiyo kauli kubwa ya mashabiki wa Simba wakijivunia uhodari wa kikosi chao kilichopambana na kutolewa kwa penalti 4-3 mbele ya Orlando Pirates katika mchezo wa robofainali ya Kombe la Shirikisho.

Simba ilimaliza dakika 90 ikiwa imelala bao 1-0 na kufanya ubao usomeke 1-1 kutokana na matokeo ya Dar es Salaam hivyo kwenda kwenye mikwaju ya penalti katika mchezo huo uliopigwa jijini Johannesburg.

Licha ya kucheza pungufu muda mrefu baada ya Chris Mugalu kuonyeshwa kadi nyekundu, Simba ikicheza kwa staili ya kujilinda muda mwingi ilionyesha ukomavu wa aina yake huku wapinzani wao wakitumia wenyeji na uzoefu wao kuamua kulazimisha matokeo. Kocha Pablo Franco alichezesha mabeki asilia watano, staili iliyombeba kumaliza dakika 45 za kwanza bila kuruhusu bao licha ya kushambuliwa muda mrefu huku Manula akionyesha ubora wake.

Pablo alianza na mabeki watano nyuma ambao ni Joash Onyango,Shomari Kapombe,Israel Mwenda,Henock Baka na Mohamed Hussein ‘Tshabalala huku Kapombe akipandishwa juu akicheza kama kiungo wa pembeni anayeingia pia kati.

Wenyeji ndio waliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya nne tu shuti la mshambuliaji Tembinkosi Lorch likapanguliwa na Manula kisha mabeki wakaokoa.

Orlando waliendelea kuliandama lango la Simba na dakika ya 29 Manula alifanya kazi nyingine bora akiokoa shuti la mpira wa adhabu kisha mabeki tena wakaokoa, adhabu iliyotokana na Lorch kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari na beki Pascal Wawa.

Advertisement

Simba walitulia na kufika kwa mara ya kwanza lango la Orlando beki Shomari Kapombe akapandisha mashambulizi lakini krosi yake ikawa ndefu kwa Mugalu na mpira kuwa wa kurushwa.

Simba ambao walianza na mabeki watano nyuma wakiwapa wakati mgumu Pirates, lango lao lilibaki tena salama dakika ya 33 wakati mshambuliaji Kwane Perrah shuti lake lililogonga mabeki wa Simba.

Mpaka mapumziko Simba bado ilikuwa salama wakitoka suluhu huku ushindi wao wa mchezo wa kwanza ukiwafanya kuongoza kwa jumla ya bao 1-0. Kipindi cha pili Orlando walirudi na nguvu ile ile wakijipanga kutafuta bao la kuongoza lakini bado walikutana na ugumu wa kupenya ngome ya Simba.

Simba walipata pigo dakika ya 59 baada ya mshambuliaji wake Mugalu kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumkanyaga beki wa Orlando ambapo baada ya marudio ya video mwamuzi Bernard Camill kutoka Shelisheli kumtoa kwa kadi hiyo.

Mapema kipindi cha kwanza Mugalu alishapewa kadi ya njano baada ya kumgonga na kiwiko beki wa Orlando, Ntsikelelo Nyauza.

Dakika moja baada ya Mugalu kutoka Orlando walipata bao la kuongoza likifungwa kwa kichwa na Perrah akimalizia krosi kali ya Bandile Shandu.

Dakika za nyongeza Simba ilinusurika kupitia marudio ya video baada ya Orlando kulalamikia tukio la Kapombe mpira kugusa mkono wake wakati kichwa cha mshambuliaji Gabadinho Mhango kugusa mkono wake.

Hata hivyo Camill alishindwa kuamua iwe penalti na kufikia maamuzi ya kumaliza mchezo huo na kuhamia kwenye penalti zilizoamua Orlando iende nusu fainali.

Simba ilipoteza penalti zake kupitia kiungo Jonas Mkude aliyepoteza ya kwanza,Offori akiicheza huku Baka akigongesha besela ambapo Kapombe,Meddie Kagere na Tshabalala walipata.

Wenyeji walipoteza penalti yao kupitia Kabelo Dlamini ambapo Manula aliicheza, huku Otto Gabadinho,Lepaso Mabasa na Offori akimfunga kipa mwenzake katika penalti ya ushindi.


KAMBI YA YANGA

Simba itarejea Tanzania huku akili zote ikizielekeza kwenye mechi ya ligi dhidi ya watani zao wa jadi Yanga itakayopigwa Aprili 30, mwaka huu.

Simba wamesisitiza kwamba kwa namna yoyote ile; “Yanga hatuwaachi.” Viongozi na benchi la ufundi wamefanya vikao mara kadhaa na kulishana yamini kwamba lazima Yanga apigwe kwenye mechi ya wikiendi ili mji utulie na wao wadhihirishe kwamba wanalitaka kombe lao. Mmoja wa viongozi wa Simba aliliambia Mwanaspoti jana usiku kwamba wameshaweka kapuni matokeo ya Sauzi, timu ikitua tu Dar es Salaam itapitiliza moja kwa moja kambini kujiandaa na mechi na Yanga.

“Hatuna muda wa mapumziko, timu itaenda moja kwa moja kambini kuanza programu maalumu za mechi ijayo,pia tutabadili kambi, kutokana na uzito wa mechi hiyo lakini hadi sasa hatujaamua tunaenda wapi lakini kufika Jumatatu jioni (leo), tutakuwa tumemaliza maandalizi yote,”alidokeza.

Lakini habari njema ni kwamba kambi zote ambazo Simba imekaa katikati ya Jiji la Dar es Salaam au uzunguni kwenye mechi zote muhimu na kubwa za hatua ya makundi ya Shirikisho zimewapa matokeo mazuri kuliko kule Mbweni wanakoishi mwaka mzima.

Kiongozi huyo alisisitiza kwamba wameamua kubadili kambi ili kuongeza morali kwa wachezaji na vilevile kujiandaa kivingine zaidi kwani mechi hiyo ya watani ni muhimu sana kwao msimu huu kuthibitisha ubora wao Tanzania na Afrika.

Licha ya kiongozi huyo kusita kuweka wazi kambi pendekezwa mpaka sasa, lakini Mwanaspoti linajua sehemu mbili ambazo Simba imepanga kuweka kambi kwenye moja ya maeneo hayo. Masaki ni kwenye hoteli ya kishua ya Element by Westin ambapo imekuwa ikikaa kwa maandalizi ya mechi za kimataifa msimu huu na ambazo zote imefanya vizuri.

Simba iliweka kambi hapo kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane ya Morocco, mabao 4-0 mbele ya USGN ya Niger na mabao 3-1 kwa Asec Mimosas ya Ivory Coast. Viongozi wanaamini kwamba licha ya utulivu wa eneo hilo lakini wana bahati kubwa wakianzia safari yao hapo.

Hoteli ya pili ambayo Simba inaweza kuweka kambi ni City Lodge, Hoteli ya kishua iliyopo Upanga Dar es Salaam ambayo nayo imekuwa ikiitumia kwenye mechi kubwa kubwa.

Kambi hii ni ile Simba iliyoitumia kujiandaa kwenye mechi ya duru ya kwanza dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa suluhu Desemba 11, mwaka jana.


REKODI

Simba imeweka rekodi ya kuwa klabu pekee ya Afrika Mashariki ambayo mafanikio yake kimataifa yameipa nchini ofa ya klabu nne kushiriki kimataifa kwa awamu mbili tofauti. Msimu ujao Tanzania itaingiza timu nne.

Advertisement