Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkwasa: Nilimnasa Betty kama utani vile-3

Picha ya Harusi ya kocha wa Taifa Satrs, Charles Mkwasa na mkewe Betty

Muktasari:

KOCHA wa Taifa Stars na nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ jana Alhamisi katika mwendelezo wa simulizi yake, aliweka bayana namna alivyokuwa mjanja kwa kujipanga kimaisha.

KOCHA wa Taifa Stars na nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ jana Alhamisi katika mwendelezo wa simulizi yake, aliweka bayana namna alivyokuwa mjanja kwa kujipanga kimaisha.

Alifunguka namna alivyojaribu kujitosa kwenye masuala ya biashara na kuchemsha, lakini pia akiweka bayana jinsi alivyolipenda soka utotoni, japo hakuota kuja kumwinua kwa kiwango alichoncho sasa.

Kadhalika aligusia alivyoanza kujitangaza kupitia Mseto. Je, maisha yake ya Mseto na ubingwa ilikuwaje na aliwezaje kutua Tumbaku mpaka Yanga na vipi kuhusu penzi lake na mkewe Betty Mkwasa? Endelea naye katika simulizi lake upate uhondo....!

 

KIFO CHA MSETO

Mkwasa anasema baada ya Mseto kutwaa ubingwa jambo la ajabu likaitokea klabu hiyo bila kutarajiwa na wengi.

“Lakini unaweza kushangaa, kwani baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa, Mseto ikafa moja kwa moja na sababu ilikuwa hivi. Kiwanda cha Tumbaku, Morogoro kiliamua kuanzisha timu yao chini ya meneja Lyatuu na kwa sababu Mseto tulikuwa na timu nzuri, ikabidi wachukue wachezaji wote pamoja na kocha wetu Mohammed Msomali tukahamia kule na kuanza maisha mapya ilikuwa mwaka 1976,” anasema Mkwasa.

“Nilicheza Tumbaku kwa muda mchache na 1978 Yanga ilinisajili na msimu wa 1979 nikaanza kucheza mechi rasmi,” anasema Mkwasa ambaye aliitwa kwa mara ya kwanza kuichezea timu ya Taifa Stars mwaka 1980.

Anasema wakati anaitwa, Taifa Stars ilikuwa imetoka kwenye mashindano ya Afcon na alianza kucheza mchezo wake wa kwanza kwenye mashindano ya Chalenji dhidi ya Sudan.

 

BUKU 7 ZAMVUTA JANGWANI

Mkwasa anaweka wazi kuwa, kwa mara ya kwanza alipewa pesa ya usajili aliposajiliwa na Yanga mwaka 1978 ambayo thamani yake ilikuwa ni Sh 7, 000 tu, wakati huo akitokea Tumbaku ya Morogoro.

“Nilianza kupata pesa ya usajili kwa mara ya kwanza, niliposajiliwa na Yanga kutoka Tumbaku ambayo ilikuwa ni Sh. 7,000 ambayo nakumbuka nililipwa kwanza Sh 4,000 na baadaye walinimalizia taratibu. Kwa sababu nilikuwa nahama na naanza maisha mapya, pesa ile niliitumia kwa kufanya ‘shoping’ ya vitu vya ndani (fenicha) kununua makochi, vitanda na vitu mbalimbali, kipindi kile klabu haikuwa ikigharamia kwa vifaa hivyo na nyingine niliitumia kwa matumizi mengine.”

 

KAZI NA SOKA

Mkwasa aliyesoma Shule ya Msingi Kilakala na Sekondari ya Forest Hill zote za Morogoro, amesoma Stashahada (Diploma) ya Biashara katika Chuo cha Biashara Dar es Salaam (CBE) ambapo kwa nyakati tofauti katika maisha yake ya uchezaji, alifanya kazi katika mashirika mbalimbali kwanza mara tu alipomaliza kidato cha nne, aliajiriwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (RDD).

Anasema aliacha kazi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa baada ya kusajiliwa n aTumbaku Morogoro ambayo pia ilimwajiri kiwandani hapo, akawa anafanya kazi anapokuwa hana majukumu ya soka na alipojiunga na Yanga Dar es Salaam, aliajiriwa Air Tanzania ambayo alifanya kuanzia mwaka 1979-2006 kabla ya kubobea kwenye ukocha.

 

ALIVYOMNASA MKEWE

Ukitaka kufahamu furaha ya Mkwasa iko wapi, wewe mtajie mkewe, Betty Mkwasa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro. Hata wakati namtupia swali kuhusu kukutana kwake na kipenzi chake sura yake inaonyesha uchangamfu isivyo kawaida huku uso ukijazwa na tabasamu zaidi ya lile lililozoeleka kwake.

Mkwasa anasema alimnasa Betty kama utani kwani hayakuwa mazingira ya soka ambayo labda mtu unaweza kusema mmojawao alimuona mwenzake na kumzimikiana na mwishowe kuja kuona. Ilikuwaje kwani?

“Nilikutana na Betty sehemu tofauti kabisa na mazingira ya soka, kipindi hicho nilikuwa mwajiriwa Air Tanzania naye alikuwa anafanya kazi Tanesco. Nakumbuka ilikuwa kati ya miaka 1982 na 1983 hivi. Na ilikuwa hivi, baada ya kazi, majira ya saa 4 mnaenda kupata chai, sisi tulikuwa tunakutana katika mgahawa mmoja, ulikuwa unaitwa Chanel Restaurant maeneo ya Posta katika jengo la Investment House Barabara ya Samora zilipokuwa ofisi za zamani za Clouds FM.

“Basi pale ndipo tulipokutana, tukafahamiana na kujuana zaidi. Si unajua vijana, unapomwona ‘mrembo’ mnayeendana kitabia na mambo mengine, roho inafurahi na ndipo tukaanzisha mahusiano, kipindi hicho, yeye hakuwa kabisa kwenye fani ya utangazaji na aliingia huko baada ya kuacha pale Tanesco.”

 

NDOA YAO

Mkwasa anafichua zaidi kuwa kuhusu mkewe: “Alienda kutangaza kwa mapenzi yake kwa sababu aliipenda fani hiyo na ukiangalia miaka ile mashirika yalikuwa yanalipa vizuri zaidi ya serikalini, lakini yeye alifanya maamuzi hayo. Pia, wakati yeye anafanya kazi hiyo ya utangazaji mimi ndiyo nilikuwa namalizia soka langu, hivyo hatukuwa tukikutana katika kazi zetu,” anafichua. Mkwasa anasema baada ya kuwa katika mahusiano yao ya muda mrefu, hatimaye walihalalishana kwa kufunga ndoa rasmi ya kanisani mwaka 1989.

“Tangu nimwoe Betty mpaka sasa ni miaka kama 26 imeshapita na mwaka jana, tulisheherekea ubarikio wa miaka 25 ya ndoa yetu (Jubilei), tukapata cheti maalumu kutoka kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni Papa Benedict XVI, kwangu ni furaha sana.”

Mkwasa na mkewe wameshafunga ndoa. Je, wamepitia changamoto zipi katika maisha yao ya mume na mkewe hadi kufikia sasaa?

Vipi kuhusu soka lake akiwa Yanga na kutamba kimataifa? Msome kesho Jumamosi katika gazeti hili la Mwanaspoti.