Mke wa Majuto awapiga biti wanaomnyemelea mumewe
Aisha Yusuf ambaye ni mke wa mwigizaji maarufu Bongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’, amewashukia wasanii wa kike ambao wamekuwa wakimmendea mume wake kimapenzi.
Akizungumza na MCL Digital, nyumbani kwao Vingunguti Jijini Dar es Salaam, Aisha amesema mara kwa mara amewakuta wasanii ambao wamekuwa wakifanya kazi na mume wake huyo kuwa na dalili za kataka kutoka nao kimapenzi.
“Nakumbuka nimeshamfuma zaidi ya mara tatu na baadhi ya wasanii ambao wakija hata nyumbani wanajidai kilichowaleta ni mambo yao ay saana, lakini kumbe kuna mambo mengine yanaendelea.
“Nilishawaonya na ninarudia tena wasithubutu kumnyemelea mume wangu, kwani bado tuna safari ndefu ya kuwalea watoto wetu wanne ambao kiumri bado ni wadogo,”amesema mama huyo wa watoto wanne.
Aisha alienda mbali zaidi na kuwaeleza wasanii hao kuwa watambue wao ni kioo cha jamii hivyo wafanye mambo yanayoendana na hilo.
Akielezea namna Majuto alivyo akiwa nyumbani tofauti na kwenye Sanaa anasema ni mtu tofauti na wanavyomuona kwenye kazi yake hiyo, japokuwa kuna wanaojisahau hata wanapofika nyumbani kuwa nae kama wapo wanaigiza.
Pamoja na umri wa miaka 70 alionao Aisha amesema ni mwanaume anayejitahidi kusaka maisha ilimradi familia yake isiadhirike.
Mbali ya watoto hao aliozaa na Aisha, pia msanii huyo ana watoto wengine sita aliozaa na mke mwingine na kuifanya familia yake kuwa na jumla ya watoto kumi.