Mgunda ashusha kitu

HUKU akimsubiri bosi wake kutua muda wowote, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amemuongeza kwenye benchi lake, staa wa zamani wa Msimbazi, Mussa Hassan Mgosi.
Straika huyo aliyekuwa anakochi timu ya vijana ya Simba, tayari ameanza kazi yake rasmi na juzi alikuwa benchi Simba ikiivaa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine.
Mgosi ambaye ni staa wa zamani wa Mtibwa na DC Motemba Pembe ya DRC, amechukua nafasi ya Selemani Matola ambaye amekwenda kwenye kozi ya ukocha Leseni A Diploma ya CAF inayoendelea kisiwani Unguja, Zanzibar.
Licha ya Mgunda kutotaka kuingia kiundani lakini habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinasema ndiye aliyemtaka Mgosi sawa na viongozi ambao walikuwa wakimfikiria kama mbadala wa Matola.
Baada ya Matola kuondoka, Mgunda ambaye ni kocha wa zamani wa Coastal Union na Taifa Stars, aliongezewa kocha wa viungo na wa makipa huku Mgunda akisubiri bosi wake ambaye Mwanaspoti linajua ni raia wa Ureno atakayechukuwa nafasi ya Zoran Maki aliyetimka.
Mwanaspoti limepenyezewa Mgosi anakaimu kwa muda wakati huu Matola yupo masomoni ambapo kozi yake hiyo itakuwa ikifanyika kwa vipindi tofauti ndani ya mwaka mmoja.
"Mgosi atakuwa anakaimu nafasi yake akiwa hayupo lakini kozi yao ni ya siku chache akirudi anaendelea na majukumu yake kama kawaida,"alidokeza mmoja wa viongozi wa Simba ambayo inafanya siri kubwa suala la Kocha Mkuu licha ya kwamba taarifa za awali zilieleza alipaswa kutua Jumatatu iliyopita.
Mgosi mbali ya kuitumikia Simba kwa mafanikio makubwa kama mchezaji, baada ya kutundika daluga aliaminiwa na kupewa timu ya wanawake akiipa mataji mawili na baadae kupewa jukumu la kuwa kocha wa timu ya vijana 'Simba B'.
Uongozi wa Simba ndio uliogharamia kozi ya Matola huku ikipanga kuwaendeleza nyota wao walioipa timu mafanikio baada ya kuacha kucheza akiwemo Erasto Nyoni na Nahodha John Bocco.