Messi alianza kuitibua real madrid mechi ya el clasico
Muktasari:
- Wachezaji wenzake wakaifunga Arsenal na hatimaye kubeba taji la ligi ya mabingwa, na katika hali ya kusikitisha Messi hakuweza kwenda kuvaa medali yake uwanjani.
TOLEO lililopita mwandishi Luca Caioli alielezea namna aliyekuwa kocha wa Chelsea, Jose Mourinho alivyochukizwa na uchezaji aliouita wa kisanii uliofanywa na Lionel Messi na kusababisha beki wa Chelsea apewe kadi nyekundu. Endelea…
Barcelona walishinda mechi hiyo, shukran kwa Eto’o kwa bao hilo pekee lakini Chelsea wao hasira zao walizihamishia kwa Messi, Mourinho alimlaumu kwa kuwa sababu ya kutolewa kwa beki wake Asier Del Horno aliyelimwa kadi nyekundu na kuifanya timu hiyo ibaki na wachezaji 10 uwanjani.
“Nini tukifanye? Tuombe waifute kadi ya Del Horno? Kumfungia Messi kwa usanii wake?
Hakuna cha kubadili matokeo, hapa unatakiwa umakini, Messi alifanya usanii, Catalonia ni nchi ya kiutamaduni, mnajua hilo na nimekuwa nikiingia kwenye kumbi za maonyesho ya sanaa mara nyingi tu na sanaa zao ni za kiwango cha juu na Messi amejifunza kwa watu walio bora katika hilo,’’ alisema Mourinho.
Bahati haikuwa upande wa timu ya Messi, katika mechi ya marudiano Machi 7, 2006, katika dakika ya 23 aliunyakua mpira kwa Robben (Arjen) lakini ghafla akaweka mkono wake wa kushoto kwenye goti, akaanguka chini, mwishowe akalazimika kuwa nje ya uwanja kwa siku 79 na kushuhudia mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa akiwa jukwaani huko jijini Paris, kwenye Stade de France.
Wachezaji wenzake wakaifunga Arsenal na hatimaye kubeba taji la ligi ya mabingwa, na katika hali ya kusikitisha Messi hakuweza kwenda kuvaa medali yake uwanjani.
Kwa wenye kumbukumbu bila shaka watakumbuka hii ndiyo mechi ambayo shabiki wa Barcelona aliingia uwanjani na kumvalisha staa wa Arsenal, Thierry Henry bendera yenye rangi ya klabu hiyo.
2006/07
Takriban mwaka mmoja baadaye, Messi hakuwa tu amepona vizuri alikuwa kama aliyeuimarisha mzimu uliokuwa ukimuandama kocha Fabio Capello.
Capello kocha mkongwe hakuwahi kushinda hata mara moja kwenye Uwanja wa Nou Camp, hakuwahi kufanya hivyo akiwa na Roma, Juventus hata Real Madrid.
Machi 10, 2006, Capello alionekana kama aliyekuwa mbioni kuuzika mzimu huo, tena katika El Clasico, mechi ya vigogo Barca dhidi ya Real Madrid, furaha iliyoje lakini alikuwa ni Messi aliyebadili matokeo, alianza kusawazisha na kufanya matokeo yasomeke 1-1 baada ya Real kuongoza kwa bao la Ruud Van Nistelrooy.
Van Nistelrooy akaongeza la pili lakini Messi tena akasawazisha kabla Real Madrid hawajaongeza bao la tatu lililofungwa na Sergio Ramos, bao lililompa Capello matumaini ya kuuzika rasmi mzuka wa kutoshinda mechi hata moja Nou Camp.
Wakati Capello akiwa na matumaini hayo na wachezaji Madrid wakiamini wamemaliza kazi, Messi, dakika ya 90 aliujaza mpira wavuni na kufanya matokeo kuwa sare ya 3-3 huku akijiwekea rekodi ya kufunga hat trick (mabao matatu) ya kwanza katika El Clasico.
Capello na mastaa wake wa Real Madrid wakawa kama watoto waliopokonywa pipi ya kijiti midomoni mwao.
Baada ya hapo Messi akaendeleza kasi yake ya mabao na inakumbukwa zaidi siku iliyoifunga Getafe katika mechi ya Kombe la Mfalme.
Wakati Messi akiendelea kuiwasha La Liga, Ronaldo naye alikuwa katika msimu mzuri na Man United katika Ligi Kuu England.
Alifanikiwa kujitofautisha na Ronaldo ambaye pia alikuwa akishutumiwa na kuandikwa mara kwa mara kwenye magazeti japo alifanya juhudi na kucheza kiwango cha juu.
Kwanza alijikuta akiingia katika kashfa ya kubaka ingawa alisafishwa katika kashfa hiyo, hapo hapo kukawa na utata uliohusu mechi ya England na Ureno katika fainali za Kombe la Dunia nchini Ujerumani mwaka 2006, mechi iliyoisha kwa Wayne Rooney kupewa kadi nyekundu na England kutolewa.
“Nimefanikiwa kuthibitisha kwamba presha zinanifanya niwe imara,’’ alisema baadaye Aprili 22, 2007 ambako alitangazwa na Chama cha Wanasoka Profesheno kuwa mwanasoka bora wa mwaka na mwanasoka bora kijana wa mwaka na hapo hapo akafuatiwa na kutwaa taji lake la kwanza la Ligi Kuu England. Ronaldo akiwa na jezi yake namba 7 mgongoni ndiye aliyetoa mchango mkubwa hadi kupatikana kwa taji hilo akishika nafasi ya tatu katika wafungaji bora mabao yake 16.
Itaendelea Jumamosi ijayo…