Mbuyu Twite sasa apata kiboko yake

Kiungo wa Yanga, Mnyarwanda Mbuyu Twite
Muktasari:
Kibopile ambaye anacheza beki wa kushoto, ameonyesha uhodari wa kurusha mipira ya namna hiyo katika michezo mbalimbali wanayocheza na kuwavutia wadau mbalimbali wa soka.
KIUNGO wa Yanga, Mnyarwanda Mbuyu Twite ndio anatambulika kuwa kinara wa kurusha mipira ya adhabu inayokwenda langoni mwa adui kama kona na Oscar Joshua wa klabu hiyo alikuwa anafuata, lakini sasa ameibuka kiboko yao anaitwa, Hamad Kibopile kutoka Mbeya City.
Kibopile ambaye anacheza beki wa kushoto, ameonyesha uhodari wa kurusha mipira ya namna hiyo katika michezo mbalimbali wanayocheza na kuwavutia wadau mbalimbali wa soka.
Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila aliliambia Mwanaspoti: “Nimemwona yule mchezaji wa Mbeya City anajua sana kurusha mipira ya adhabu ambayo haina tofauti kabisa na kona. Ni kama vile ambavyo Mbuyu anavyorusha, kuanzia pembeni na inafika kabisa kwenye 18 bila wasiwasi.”
Kiungo tegemeo wa Mbeya City, Anthony Matogoro amesema: “Jamaa ana upeo wa kurusha mipira ambayo huwezi kutofautisha kabisa na kona na ina nguvu kama ambavyo Mbuyu wa Yanga anavyorusha.”
Kibopile alisema: “Ukiwa na malengo unafanikiwa, nimefanyia mazoezi ndiyo maana nimefanikiwa.” Mbali na uhodari huo wa mipira ya kurusha, Kibopile ni mkali pia katika mipira inayokufa.