Mayele: Mtanikuta huku

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele ambaye ameitwa kwenye kikosi cha timu ya DR Congo kinachojiandaa na mechi za kufuzu Afcon dhidi ya Mauritania Ijumaa hii, amesema hatarudi tena Tanzania ataungana na Yanga huko huko.
DR Congo mara baada ya mchezo wao wa kwanza kukamilika Ijumaa hii watakuwa na kibarua kingine Machi 28 mchezo wa marudiano ugenini na baada ya hapo atawasubiri Yanga wanaokwenda kuvaana na TP Mazembe.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayele alisema ameshawasiliana na uongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kuwasilisha ombi hilo hivyo hataweza kujiunga na wenzake mara baada ya kulitumikia taifa lake na atabaki kuwasubiri Yanga tayari kuwavaa TP Mazembe Aprili 2.
“Tunakutana na TP Mazembe Aprili 2 na mimi nitakuwa na mchezo wa marudiano na Mouritania ugenini Machi 28, nitarudi na timu baada ya mechi Congo muda utakuwa umeshasogea sitaweza kurudi Tanzania nitaungana na wenzangu huku;
“Suala la kwamba ni mchezo wa kukamilisha ratiba linabaki kwa mashabiki sisi kama wachezaji tunakwenda kupambana kuhakikisha tunapata matokeo ya ushindi ili kuendelea kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuongoza kundi.”
Alisema anawaheshimu TP Mazembe na hawataingia kwenye mchezo huo kwa kujiamini kutokana na matokeo waliyoyapata kwa Mkapa wataingia kwa kuamini kuwa ni mchezo ambao utaamuliwa ndani ya dakika 90.