Matola afichua siri za Banda, Sakho

WAKO moto! Ndivyo unaweza kusema kwa mastaa wawili wa Simba, Mmalawi Peter Banda na Msenegal Pape Sakho kutokana na kiwango walichokionyesha kwenye mechi mbili za mwisho za timu hiyo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola aliyefichua siri ya ubora wao.

Wawili hao kwa pamoja katika mechi hizo ambazo Matola ameiongoza wakati akisubiri ujio wa kocha mkuu baada ya kuachana na Mhispania Pablo Franco, wamehusika kwenye mabao yote sita dhidi ya Mbeya City na KMC.

Sakho amehusika kwenye mabao matano, akifunga mawili mechi ya Mbeya City huku mechi dhidi ya KMC akifunga moja na kutoa asisti mbili huku Banda akifunga bao moja dhidi ya Mbeya City.

Akizungumzia ubora wa vijana hao ambao walianza msimu kwa kusuasua wakiwa wageni kwenye ligi, Matola amefichua imani na muda wa kucheza ni miongoni mwa sababu za kuwafanya wawe bora.

“Wote ni wachezaji wazuri pia vijana wanahitaji kuaminiwa ili wafanye vizuri zaidi. Kama unavyoona kwenye mechi hizi mbili nimewaamini na kuwapa nafasi na wwameleta matokeo mazuri,” alisema Matola na kuongeza;

“Wakati mwingine presha za timu hizi zinachangia wachezaji kutofanya vizuri lakini taratibu wanazoea na naamini kwenye mechi zijazo watakuwa bora zaidi na wataisaidia Simba.”

Licha ya kuwa na kiwango bora, Banda alieleza bado anahitaji kupambana zaidi ili kufanya mazuri kwa Simba na mashabiki wake kwa jumla.

“Nilikuwa majeruhi sasa nimepona, nahitaji kuendelea kufanya vizuri ili niwe bora zaidi yas hapa jambo nalioamini baada ya muda mfupi nitakuwa imara zaidi,” alisema Banda.

Simba kwa sasa inacheza mechi za Ligi ili kukamilisha ratiba baada ya kujihakikishia kumaliza nafasi ya pili chini ya mabingwa Yanga na kimya kimya inaendelea na usajili kuhakikisha msimu ujao inarejea kwenye makali yake ya misimu minne iliyopita mfululzo ikitwaa makombe yote ya ligi.