Mastaa Simba kumwagiwa noti

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Miongoni mwa vitu alivyozungumza Kajula yupo kwenye nafasi hiyo kama daraja la kuunganisha wachezaji, benchi la ufundi na uongozi kutatua changamoto na kila mmoja kufanya kazi kwenye mazingira sahihi.

KIKOSI cha Simba kilikuwa na mchezo mgumu wa mzunguko wa pili kwenye Ligi Kuu Bara jana  kucheza dhidi ya Singida Big Stars na mchezo ulimalizika kwa ushindi wa mabao 3-1 huku simba ikifikisha alama 53.

Lakini mapema juzi Ofisa Mtendaji mpya wa klabu hiyo, Imani Kajula aliwaibukia mastaa kambini na kuwaahidi neema ikiwamo kuwamwagia noti za kutosha.

Kajula alitembelea kambi hiyo iliyopo Mbweni kisha kufanya kikao kisichopungua dakika 30, kikiwa na wachezaji na benchi la ufundi ndipo wachezaji wakakumbushia fedha wanazodai kutokana na aahdi ya kyuifikisha Simba makundi ya Ligi ya Mabingwa na kuahiwa watalipwa.

Kwenye kikao Kajula alijitambulisha kwa wachezaji, benchi la ufundi pamoja na majukumu ya kazi anayokwenda kuyafanya kwani tangu amepata nafasi hiyo hakuwahi kuzungumza na wachezaji ingawa kuna baadhi  anafahamiana nao alishawahi kufanya nao kazi kwa pamoja miaka ya nyuma.

Miongoni mwa vitu alivyozungumza Kajula yupo kwenye nafasi hiyo kama daraja la kuunganisha wachezaji, benchi la ufundi na uongozi kutatua changamoto na kila mmoja kufanya kazi kwenye mazingira sahihi.

Baada ya hapo aligusia chini ya uongozi wake kwanza atakwenda kulipa posho za wachezaji walizoahidiwa wakati wanafuzu hatua ya makundi Ligi ya mabingwa Afrika msimu huu ambazo hadi sasa hawajapata.

Wachezaji walielezwa kabla ya kupanda ndege kwenda Guinea kucheza mechi ya mashindano hayo dhidi ya Horoya kila mmoja atakuwa amepata bonasi aliyostahili kupata baada ya kufuzu hatua ya makundi.

Wachezaji walielezwa huenda posho hizo zilichelewa kutokana na sababu ya mabadiliko ya uongozi ila jambo hilo haraka linakwenda kufanyiwa kazi na malipo kufanyika mapema kila mmoja kupata anachostahili.

Jambo lingine wachezaji walielezwa kila mmoja anatakiwa kupambana kwenye mechi zote na timu kufikia malengo yake ya kupata ushindi na kushinda mataji yaliyokuwa mbele yao.
Wachezaji walisisitizwa kupambana vya kutoka kwenye Ligi ya mabingwa Afrika kuanzia hatua hii ya makundi na kama ikitokea kuna ambaye atafanya vizuri na kuhitajika timu nyingine kubwa Afrika na Ulaya kama uongozi wakikubaliana wapo tayari kumuachia.

Lingine wachezaji walielezwa imebaki michezo tisa kwenye Ligi Kuu Bara wanatakiwa kupambana na kuhakikisha wanashinda yote ili kuangalia msimu huu watamaliza kwenye nafasi ya ngapi.
Jambo lingine waliahidiwa wachezaji na benchi la ufundi kila kitu wanachostahili kupata watakuwa wanapata kwa wakati kama walivyokubaliana ili timu iweze kufanya vizuri kwenye michezo yote.

Mwanaspoti lilimtafuta Kajula aweze kuzungumzia hasa suala la kucheleweshewa  kwa bonasi ya wachezaji ya kufuzu hatua ya makundi lakini simu yake tangu asubuhi ya jana saa tatu hadi saa saba mchana ilikuwa inatumika.

Lakini mmoja wa  watu wa ndani ya Simba ambao walihudhulia kikao hicho alilidokeza Mwanaspoti kwa kusema; "Mkuu anataka timu ifanye vizuri na ndio maana kila mtu alikuwa huru kuzungumza kwenye kikao."

Mwanaspoti linafahamu Simba imekuwa na kawaida ya kuweka ahadi kubwa kwa wachezaji wao kwenye mechi za kimataifa ili kuwapa morali ya kufanya vizuri.