Marefa wa VAR za Simba, Yanga CAF hawa hapa

Muktasari:

  • Dimbiniaina naye atakuwa anakuja Tanzania kwa mara yapili katika siku za hivi karibuni kwani yeye ndio alikuwa mshika kibendera namba moja kwenye mchezo wa ufunguzi wa African Football League kati ya Simba na Al Ahly uliomalizika kwa sare ya 2-2.

SAA chache kabla Simba kushuka uwanjani kuvaana na Al Ahly ya Misri katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limewaweka bayana marefa wa wasaidizi watakaosimamia VAR, ambapo Dahane Beida kutoka Maurtania atasimamia shoo hiyo ya Simba.

Beida atasaidiwa na Ahmad Imtehaz kutoka Mauritius katika mechi kati ya Simba na Al Ahly itakayopigwa kesho kuanzia saa 3:00 usiku Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Dahane mwenye umri wa miaka 32, ni miongoni mwa waamuzi vijana wanaofanya vizuri kwa sasa  na hii sio mara yake ya kwanza kuchezesha mechi iliyokutanisha vigogo hawa, kwani alikuwa ndio mwamuzi wa kati kwenye mechi ya ufunguzi wa michuano mipya ya African Football League kati ya Simba na Ahly.

Dahane Beida

Kwa upande wa Yanga, mwamuzi kiongozi kwenye VAR ni Mahmoud Ashor na Mahmoud Elbana wote kutoka Misri.

Mwamuzi wa kati, katika mechi ya Simba atakuwa ni Abongile Tom kutoka Afrika Kusini ambaye hii inakuwa ni mara ya pili kusimama kwenye mechi ya Simba katika kipindi cha hivi karibuni.

Tom ndio alikuwa mwamuzi kwenye mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu kati ya Simba na Wydad Casablanca iliyopigwa kule Morocco ambako Simba ilifungwa bao 1-0.

Aliwahi kuja Tanzania Novemba mwaka jana kusimamia mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na Morocco.

Huyu atasaidiwa na Zakhele Thusi Granville atakayekuwa mshika kibendera namba moja na Dimbiniaina Andriatianarivelo namba mbili.

Dimbiniaina naye atakuwa anakuja Tanzania kwa mara yapili katika siku za hivi karibuni kwani yeye ndio alikuwa mshika kibendera namba moja kwenye mchezo wa ufunguzi wa African Football League kati ya Simba na Al Ahly uliomalizika kwa sare ya 2-2.

Kwa upande wa waamuzi wa kati, mechi ya Yanga na Mamelodi Sundowns, atakuwapo Amin Mohamed Omar kutoka Misri aliyesimama katika mechi ya AFCON kati ya DR Congo na Tanzania, kule Ivory Coast na Jumamosi atasaidiwa na Mahmoud Ahmed na Ahmed Hossam wote kutoka Misri.

Yanga na Mamelodi zitakutana pia kwenye mechi ya robo fainali siku ya Jumamosi kuanzia saa 3:00 usiku pia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na zitarudiana Aprili 5 mjini Pretoria, Afrika Kusini.