MANSOUR VARDY: Kejeli za mashabiki zinanikosesha utulivu
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo mwenye mabao 15 katika mechi 21 alizocheza, amesema mashabiki wake wamezoea kumwona akifunga kila mechi na asipofanya hivyo wanamkejeli kwa maneno mabaya, hivyo inamuwia vigumu wakati mwingine.
KINARA wa mabao Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, kutoka Black Sailors, Mansour Omar Kombo 'Vardy' amesema presha ya mashabiki ndiyo sababu kubwa inayomfanya ashindwe kutupia mabao kwenye mechi muhimu.
Mshambuliaji huyo mwenye mabao 15 katika mechi 21 alizocheza, amesema mashabiki wake wamezoea kumwona akifunga kila mechi na asipofanya hivyo wanamkejeli kwa maneno mabaya, hivyo inamuwia vigumu wakati mwingine.
"Kuna wakati presha za mashabiki zinanifanya nipoteze utulivu kwenye mechi muhimu, ndiyo sababu najikuta natengeneza nafasi lakini sipati bao," amesema Vardy.
Mshambuliaji huyo, amesema anajisikia vizuri sana kuona timu yao ina muelekeo mzuri wa kupanda daraja kushiriki Ligi Kuu Zanzibar licha ya changamoto mbalimbali wanazopitia, haziwakatishi tamaa.
Amesema uongozi wa timu hiyo umekuwa chachu kwa wachezaji kupambana na kutoa matokeo mazuri kila mechi kwani kati ya mechi 21 ilizocheza, imepoteza moja na kushinda 18, ikitoa sare mbili.
Mechi kati ya Black Sailors na Sebleni ambayo timu hiyo iliibuka na ushindi wa bao 1-0, amesema hiyo ni miongoni mwa mechi ngumu kwake msimu huu kwa sababu alikosa mabao mengi.
Hivyo, mshambuliaji huyo ametoa wito kwa mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuiunga mkono kwani ina kiu ya kucheza Ligi Kuu na dalili zimeshaanza kuwa njema upande wao hadi sasa.