Msako nne bora ZPL, KVZ yakwea kileleni
Muktasari:
- Kipigo hicho kimeifanya timu hiyo kushuka kutoka nafasi ya tatu hadi ya nne ikiipisha Uhamiaji, upande wa Polisi bado ipo kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja.
MSIMAMO wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kwa nafasi nne za juu, moto unawaka baada ya mechi za raundi ya 21 kuchezwa na kuleta picha mpya tofauti na ilivyokuwa awali.
Hiyo imetokana na mechi kati ya Uhamiaji na Junguni iliyochezwa Alhamisi ya Aprili 2, 2026, kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, kuwa na ushindani huku Uhamiaji ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mchezaji Abel Simwinga (dakika ya pili) na Abdulhafidh Kibobea, 80, na kuipa timu hiyo pointi tatu ugenini.
Katika mechi nyingine, KVZ iliifunga Mafunzo mabao 3-1 na kukaa kileleni kwa kufikisha pointi 40, ikifuatiwa na Zimamoto yenye pointi 39 baada ya kupata sare ya 1-1 dhidi ya Kipanga, wakati Uhamiaji yenye pointi 39 iliyoshinda 2-0 dhidi ya Junguni ikiwa ya tatu, huku Fufuni ikitoka kileleni na kushuka hadi nafasi ya nne ikibaki na pointi 38 baada ya kufungwa 2-0 na Polisi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh amesema ugumu wa mechi ndiyo sababu ya kuvuna alama hizo zilizofanikisha kupanda hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi.
Amesema siri ya ushindi huo ni wachezaji kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kucheza katika muunganiko mzuri uliochangia kupatikana kwa mabao hayo.
"Kwa kawaida mechi zinazotokea kisiwani Pemba ligi ikifika hatua ya lala salama zinatoa ushindani mkubwa na hapo ndipo ugumu unapoanzia," amesema Abdul.
Amesema kwa mantiki hiyo timu inapopata alama tatu kutoka kwa timu za Pemba siyo rahisi bali ni kazi imefanyika ndiyo maana wanajivunia hilo.
Kwa upande wa Mlandege, ilitembeza kipigo cha mabao 5-2 dhidi ya New Stone Town kwenye Uwanja wa Mao B, Mjini Unguja, ikiendelea kusalia nafasi ya saba.
Akizungumza baada ya mechi hiyo iliyochezwa Aprili 2 mwaka huu, Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China amesema mbinu ya timu kuchezesha wachezaji ambao hawajatumika kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo wamepata nafasi ya kuonesha ubora wao na kuvuna alama tatu.
Hata hivyo, kocha huyo amesema haridhishwi na nafasi iliyopo timu hiyo kwa sasa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar, ndiyo maana inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inashinda mechi zake ili kujiweka pazuri.
Mlandege ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar ikibeba kombe msimu wa 2024-2025 na sasa ipo nafasi ya saba ya msimamo huo na jumla ya pointi 34 kati ya mechi 21 ilizocheza.
Wakati hayo yakijiri, kwa waliokuwa vinara wa ligi hiyo mzunguko wa kwanza Fufuni imepokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Polisi inayopambana kubaki ligi Kuu msimu huu.
Kipigo hicho kimeifanya timu hiyo kushuka kutoka nafasi ya tatu hadi ya nne ikiipisha Uhamiaji, upande wa Polisi bado ipo kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja.