Makocha 17 wahitimu kozi soka la vijana Mwanza, Kaijage awapa mbinu
JUMLA ya makocha 17 kutoka mikoa ya Mwanza na Tabora wamehitimu mafunzo ya siku 10 kozi ya soka la vijana (Grassroots) inayotolewa na Shirikisho la soka nchini (TFF) kwa kushirikiana na lile la Kimataifa (FIFA).
Kozi hiyo iliyoandaliwa na Chama cha makocha (TAFCA) mkoa wa Mwanza ilianza Februari 25 na kumalizika leo Machi 5 katika shule ya Mirongo jijini Mwanza ikishirikisha wachezaji wa zamani, waandishi wa habari, waamuzi na walimu wa shule.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Rogasian Kaijage amesema mkoa wa Mwanza umekuwa na changamoto ya kutoa makocha kwani hawataki kupata elimu huku akiwataka wahitimu hao kujiboresha na kuwa na uwezo wa kufanya kazi Kwa vitendo ili kuponya tatizo la kukimbilia makocha wa nje.
"Sasahivi hakuna kubembeleza mtu kila mwenye nia ya kutaka kufanya hii kazi asome lazima tusome tupate elimu tuwe mahiri tufanye kazi kwa utaalam na usahihi na tujiboreshe, nafanafurahi kuona waandishi wa habari wanahudhuria ni jambo zuri kwa sababu watasaidia kufundisha wengine," amesema Kaijage.
Katibu Mkuu TAFCA mkoa wa Mwanza, George Msengi amesema kozi hiyo itawapa mwanga na msingi kwani ukocha ni kazi na taaluma yenye thamani kubwa, huku akiwataka kutotunza vyeti ndani bali wavifanyie kazi ili kuongeza uelewa na kukua.
"Kazi yoyote ili uifanye kwa ufanisi ni lazima uwe umeisomea umefahamu maadili na misingi yake siyo mazoea tu kisa ulicheza zamani, huwezi kufundisha mpira kwa usahihi kama huna taaluma hii tusiishie kuwa walimu tuwe wabunifu tuwe makocha," amesema Msengi.
Miongoni mwa waliohitimu mafunzo hayo ni wachezaji wa zamani Amir Maftaha, Robert Magadula, Ladislaus Mbogo na mwandishi wa habari Dickson Mpilipili, ambapo Maftaha amesema
wachezaji wengi waliocheza mpira wanaamini baada ya kustaafu basi wanaweza kufundisha huku akiamini alichokipata na uzoefu alionao vitamsaidia kufikia malengo ya ukocha.