Makambo: Nakuja Yanga kuwajaza

STRAIKA kipenzi wa mashabiki wa Yanga, Heritier Makambo ametamka kauli ambayo mashabiki wa klabu hiyo walikuwa wanaisubiri kwa hamu.

Makambo ambaye ni raia wa DR Congo aliyemwagana na AC Horoya ya Guinea, ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka nje kidogo ya Jiji la Kinshasa kwamba: “Nakuja Yanga.” Mwanaspoti linajua kwamba kila kitu baina ya Yanga na mchezaji huyo kipo kwenye hatua za mwisho na baadhi ya vigogo wamepania kumshusha Dar kwa kishindo ingawa kuna baadhi wanaihofia Azam huenda ikatia mkono.

Mchezaji huyo amekiri kwamba kuna mazungumzo mazuri baina yake na Yanga na kama yakikamilika muda wowote atakuja kuishia pale alipoishia maana Jangwani ni nyumbani kwake.

Kabla ya kutimka Yanga akiuzwa Horoya, Makambo alikuwa staa mkubwa akifunga mabao 17 katika ligi ambapo licha ya Yanga kukosa ubingwa wala kombe lolote, lakini aliibuka kuwa mfungaji bora wa kikosi hicho cha kocha wa wakati huo, Mwinyi Zahera Mkongomani mwenzake.

Makambo aliuzwa Horoya kwa Euro 70,000 akiwa ameitumikia Yanga mwaka mmoja pekee katika miaka miwili aliyosaini ambapo hata hivyo akiwa nchini Guinea alishindwa kutamba katika miaka yake miwili ya kwanza kabla ya wiki hii kuvunja mkataba na mabingwa hao wa nchini humo na wakaachana kiroho safi akasepa zake DR Congo.

“Siwezi kukataa kurejea Yanga, hiyo ni klabu ambayo ilinitambulisha karibu sehemu kubwa, nawakumbuka sana watu wa Yanga, ni kweli nipo katika mazungumzo na viongozi,” alisema Makambo ambaye alitamba na staili yake ya kushangilia ya kuwajaza akipiga viganja vyake viwili huku mikono akivinyoosha kila alipofunga bao.

“Yanga ni nyumbani nikikamilisha na kurudi sasa ni kama nakuja kuendelea nilipoishia na sasa najua kila kitu kwamba wana timu nzuri ambayo inashinda na watu wanaojua kufunga, kazi ambayo sina wasiwasi nayo,” alisema Makambo ambaye yupo kwao DR Congo akipumzika kwa muda mfupi na familia yake, lakini pia akisubiri simu ya kumalizia dili hilo kutoka kwa Injinia Hersi Said.

“Nipo na familia tu na-pumzika kidogo baada ya kusitisha mkataba wangu, niliona ni bora niondoke ili nisije kupotea zaidi. Nipo hapa nasubiri pia simu ya bosi Hersi (Said), ni mtu mzuri sana tumekuwa tukizungumza vizuri mpaka sasa.”


AWAKUBALI KISINDA, MUKOKO

Akizungumzia uwepo wa Wakongomani wenzake katika kikosi cha Yanga, winga Tuisila Kisinda na kiungo Mukoko Tonombe, Makambo alisema hiyo ni hatua kubwa kwa Yanga kwani sasa ina wachezaji wakubwa waliokomaa.

“Nilikuwa nacheza nao Congo wakati nikiwa hapa Congo, ingawa tulikuwa timu tofauti, nawafahamu sana Kisinda ni winga mzuri anayejua kazi yake, mshambuliaji yeyote atafurahi kucheza naye, nitafurahi kama nitaungana nao ili tufanye kazi vizuri ndani ya Yanga,” alisisitiza.

Makambo alikuwa kipenzi cha viongozi wa Horoya, lakini mfumo wa benchi la ufundi ukamgomea na akajikuta akisota benchi kwa muda.

Mwanaspoti linajua pia kwamba Horoya iliwahi kukataa dili la Yanga kuhusu Makambo mwanzoni mwa mwaka huu wakiamini ishu zitakaa sawa.