Madenti wapiga pedeli wafanya kweli
Muktasari:
- Omari alimaliza mbio hizo zilizoandaliwa na Masjid Noor Kange za kilomita 15 kwa kutumia saa 1:53:30 akifuatiwa na Adam Abdul aliyekimbia kwa saa 1:53:33, huku Athuman Aziz akishika nafasi ya tatu kwa kukimbia kwa saa 1;53;40.
OMARI Idd, mwanafunzi wa darasa la tano wa Shule ya Msingi Kange ameibuka bingwa wa mbio za baiskeli za kuadhimisha mwaka mpya wa Kiislamu wa 1446 zilizofanyika Kange jijini hapa.
Omari alimaliza mbio hizo zilizoandaliwa na Masjid Noor Kange za kilomita 15 kwa kutumia saa 1:53:30 akifuatiwa na Adam Abdul aliyekimbia kwa saa 1:53:33, huku Athuman Aziz akishika nafasi ya tatu kwa kukimbia kwa saa 1;53;40.
Nafasi ya nne, ilikwenda kwa Issa Rashid aliyekimbia kwa saa 1:54:00, huku Amani Hussein alimaliza nafasi ya tano akitumia saa 1:54:20 akifuatiwa na Athuman Imma, Idrisa Mussa, Nasri Gama, Muhud Mutwalib Abdul Aziz na Ally Rashid.
Katibu wa Masjid Noor, Juma Nyange alisema lengo la mashindano hayo ni kukuza vipaji vya vijana katika michezo na kuadhimisha mwaka mpya kwa Kiislamu.
“Kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Mkoa wa Tanga tumeazimia kuboresha zaidi mchezo huu kwa mwaka ujao ambapo tutapanua kwa kushirikisha vijana bla kubagua dini zao, tutaongeza kilomita na zawadi zitakuwa kubwa zaidi," alisema Nyange.
Katibu wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Tanga, Muzamiru Mafita aliahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali katika mashindano hayo kwa kuwa yanasaidia kuhamasisha na kuhuisha mchezo huo ambao ni ajira kubwa kwa vijana.
“Mbio za baiskeli ni mchezo ambao umekuwa ukiwawezesha vijana kupata fursa ya kwenda nchi mbalimbali Duniani kushiriki mbio hizo kwa hivyo tuna kila sababu ya kuwaandaa wakiwa wadogo," alisema Mafita.