Maamuzi magumu Simba kufumua ukuta wote

Thursday March 12 2020
pic simba

SIMBA wamekubaliana kwa kauli moja kwamba lazima wafanye mabadiliko makubwa kwenye sehemu ya kati ya safu yao ya ulinzi kabla ya kutia mguu katika Ligi ya Mabingwa Afrika Agosti mwaka huu.

Wekundu wa Msimbazi wamefanya uamuzi huo baada ya kukerwa na ufanisi wa safu hiyo hasa kwenye mechi mbili za watani wa jadi msimu huu ambapo moja waliambulia sare ya mabao 2-2 na ya pili wakalala bao 1-0.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ndani ya Simba ni kwamba baada ya mechi ya Yanga wikiendi iliyopita wamekubaliana kwamba usajili wa kwanza kabisa kufanyika kuanzia sasa ni mabeki watatu (wawili kati na mmoja kulia).

Lakini kama hiyo haitoshi mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba alisema kwa sasa wanafuatilia kwa karibu mawasiliano ya wachezaji wao ili kuangalia kama kuna hujuma yoyote katika safari ya ubingwa.

Anasema Bodi ilikutana na kocha wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck akawaambia; “Sven anataka mabeki wasiopungua watatu, wote wawe na uwezo mkubwa wa kucheza katika nafasi hiyo ila mmoja kati ya hao awe anaweza kucheza mlinzi wa kulia.”

“Jambo jingine ambalo alieleza kwetu ni kuwa wachezaji wengi wa Simba wameonekana kutumika sana na umri umekwenda, kwa maana hiyo anahitaji kusajili pia wachezaji vijana kuanzia katika eneo hilo la safu ya ulinzi na kuwapata waliokuwa bora zaidi ya Erasto Nyoni na Pascal Wawa ambao wanacheza mara kwa mara.

Advertisement

“Kwetu uongozi tumeyapokea mapendekezo yake na ambalo tumemuahidi tutampatia bajeti kubwa ya pesa ili kusajili mabeki hao watatu wa maana ambao anawataka kulingana na sifa au mahitaji yake ili kuwa na safu bora ya ulinzi jambo ambalo hata kwetu tumeliona kuwa nafasi hiyo ina shida tangu msimu huu kuanza,” alidokeza kiongozi huyo.

Habari zinasema kwamba tayari Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba ametoa kazi kwa mawakala wakubwa wa Afrika wamtafutie mashine hizo tatu za maana na kama ikiwezekana wasainishwe kabla hata msimu haujamalizika.

Mwanaspoti limebaini kuwa uongozi wa Simba unaweza kuachana na mabeki Mbrazili Tairone Santos na Yusuph Mlipili ambao wamekuwa hawatumiki mara kwa mara kwenye kikosi hicho kama ilivyo kwa Nyoni, Wawa na Kennedy Juma ambao wanacheza kwenye nafasi hiyo lakini na wao wawili kati yao safari itawakumba.

Simba jana Jumatano walicheza mechi ya mzunguko wa 28, wa ligi dhidi ya Singida United na katika kikosi chao kilikuwa na mabadiliko hasa katika eneo la beki wa kati walipomkosa Nyoni ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili baada ya kuumia mguu pamoja na Kennedy ambaye ameomba ruhusa ya kwenda kwao kumaliza matatizo ya kifamilia.

Kagere ainasa rekodi ya Tambwe

STRAIKA Meddie Kegere wa Simba jana aliandika rekodi yake ya kwanza tangu aanze kucheza soka nchini kwa kufunga mabao manne, wakati timu yake ikiifumua Singida United 8-0 na kuifikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Amissi Tambwe katika misimu miwili tofauti enzi akikipiga Simba na Yanga.

Tambwe aliyevunja mkataba wake na FC Fanja ya Oman, alifunga mabao manne kwa mara ya kwanza mwaka 2013 akiichezea Simba wakati wakiifumua Mgambo JKT mabao 6-0 kabla ya kurudia tena 2015 alipokuwa Yanga walipoichakaza Coastal Union ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kwa mabao 8-0.

Hata hivyo, Kagere ambaye ndiye kinara wa mabao na anayecheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili alifanya yake jana kwa kufunga mabao hayo na kuondoka na mpira ikiwa ni hat trick yake ya kwanza msimu huu na ya pili kwake nchini akiipaisha Simba ijikite kileleni na alama zao 71 baada ya mechi 28.

Kagere aliyefikisha mabao 19, alitupia kambani katika dakika ya 2, 26, 42 na 71, huku mabao mengine ya mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja yakizamishwa nyavuni na Deo Kanda aliyefunga mawili dakika ya 13 na 19, John Bocco na Shiboub Sharafeldin nao wakitupia moja moja dakika za 20 na 60.

Simba iliyotoka kupoteza mbele ya Yanga Jumapili iliyopita, ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo ambao Singida ilionekana wazi ni kama haikujiandaa. Mkongwe Haruna Moshi ‘Boban’ aliidhoofisha Singida kwa kupewa kadi nyekundu dakika ya 58 kwa kumpiga kiwiko Aishi Manula.

Advertisement