Lunyamila anateseka
Lunyamila akiwa amelala kitandani hospitalini .PICHA|MAKTABA
Muktasari:
Ndugu wa Lunyamila aliyemfikisha hospitali hapo aitwaye Lameck John, aliliambia Mwanaspoti kwamba Lunyamila alianza kujisikia vibaya juzi Jumapili na jana Jumatatu asubuhi hali yake ilibadilika ndipo alipomwahisha hospitali.
WINGA wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Edibily Lunyamila, amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala na anapumua kwa msaada wa mashine.
Mwanaspoti jana Jumatatu mchana lilimshuhudia Lunyamila akiwa amelala katika kitanda namba 18 cha wodi ya wanaume katika hospitali hiyo ya mkoa wa kitabibu wa Kinondoni.
Kwa mujibu wa Daktari, Madirisha Pascal, aliyempokea na kumpatia huduma ya kwanza winga huyo wa zamani, Lunyamila anasumbuliwa na tatizo la kifua ambalo linamfanya ashindwe kupumua vizuri.
“Sasa anapumua kwa msaada wa mashine na bado tunaendelea kumfanyia uchunguzi ili kubaini nini kinachomsumbua zaidi,” alisema Pascal.
Ndugu wa Lunyamila aliyemfikisha hospitali hapo aitwaye Lameck John, aliliambia Mwanaspoti kwamba Lunyamila alianza kujisikia vibaya juzi Jumapili na jana Jumatatu asubuhi hali yake ilibadilika ndipo alipomwahisha hospitali.
“Alikuwa analalamika hawezi kupumua na kifua kinamsumbua pia mbavu zilikuwa zikimuuma, baada ya majibu ya vipimo tutajua kinachomsumbua zaidi,” alisema Lameck.
Lunyamila hakuweza kuzungumza na mwandishi wa habari hii kwani alikuwa amelala.
Lunyamila aliyeichezea Yanga kwa mafanikio katika miaka ya 1990, amewahi kuisaidia Yanga kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998.