Kocha Kurasini Heat akosa mpinzani urais BD, kamati yaonya
Muktasari:
- Uongozi mpya utakaoingia madarakani utakuwa na jukumu la kuandaa na kusimamia Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA) ambayo ilikuwa ianze tangu Mei, lakini ikasogezwa mbele kupisha uchaguzi.
Wakati Kamati ikionya ikisisitiza kuwa usaili wa wagombea kwenye uchaguzi mkuu wa Chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD) hautamuonea au kumpendelea yeyote, kocha Shendu Mwagalla wa Kurasini Heat amekosa mpinzani kwenye kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi huo.
Shendu ambaye aliiongoza Kurasini Heat kutwaa ubingwa wa RBA msimu huu kama atapenya kwenye usaili keshokutwa, atapigiwa kura ya ndiyo au hapana kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Julai 10.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Gosbert Boniface amesema usaili kwa wagombea wote utaanza saa 2 Asubuhi kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Sa;aam.
"Haturuhusu kumpitisha mgombea asiye na sifa, tunachokitaka ni BD kupata uongozi makini, hivyo mchakato wa usaili hautambeba wala kumpendelea yeyote," amesema.
Amesema utaratibu wa kupiga kura pia kwenye uchaguzi huo utakuwa ni tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma.
"Zamani yoyote alikuwa anakuja na kupiga kura, lakini sasa ni zile klabu tu zilizosajiliwa na msajili wa BMT na ziwe zinazocheza mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam bila kujali iko daraja lipi.
"Wapiga kura wengine ni wajumbe wa bodi ambao ni rais, katibu mkuu na makamishna wanaomaliza muda wao na mwenyekiti na katibu mkuu wa chama waamuzi, ambao idadi yao tutaitoa Julai Mosi," amesema.
Amesema nafasi kadhaa zimetapa wagombea mmoja mmoja, ikiwamo ya urais ambayo inawania na Shendu pekee baada ya Okare Emesu kumaliza muda wake.
Kwa mujibu wa kanuni, endapo Shendu atashinda, atalazimika kuachia ngazi kuinoa Kurasini Heat inayojiandaa kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya kikapu Afrika (BAL).
Nafasi nyingine yenye mgombea mmoja ni ile ya makamu inayowaniwa na Malale Masanywa wa klabu ya Outsiders na Kamisheni ya wanawake ambayo inawania na Fatuma Yasoda.
Nafasi ya katibu mkuu ina wagombea wawili sawa na walio kwenye kamisheni ya mipango na maendeleo, wakati kamisheni yenye wagombea wengi ni ya watoto na maendeleo ya michezo shuleni yenye wagombea watatu.