KMC rasmi imeshuka daraja baada ya misimu nane Ligi Kuu
Muktasari:
- Hatima ya timu hiyo ya Dar es Salaam ilithibitishwa baada ya kufungwa bao 1-0 na TRA United, matokeo yaliyoiweka KMC katika nafasi ngumu ikiwa na alama tisa pekee baada ya kucheza mechi 26 za msimu huu. Ikiwa zimebaki mechi nne kumaliza msimu, KMC inaweza kufikisha alama 21 tu iwapo itashinda michezo yote iliyosalia.
Klabu ya Soka ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC) imeshuka rasmi daraja na itashiriki Ligi ya Champion-ship msimu ujao baada ya kudumu kwa misimu minane mfululizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hatima ya timu hiyo ya Dar es Salaam ilithibitishwa baada ya kufungwa bao 1-0 na TRA United, matokeo yaliyoiweka KMC katika nafasi ngumu ikiwa na alama tisa pekee baada ya kucheza mechi 26 za msimu huu. Ikiwa zimebaki mechi nne kumaliza msimu, KMC inaweza kufikisha alama 21 tu iwapo itashinda michezo yote iliyosalia.
Hata hivyo, idadi hiyo ya alama haitatosha kuiokoa kutoka eneo la kushuka daraja. Kiwango cha juu kabisa wanachoweza kufikia ni kumaliza juu ya Tanzania Prisons, ambao kwa sasa wako nafasi ya 15 wakiwa na alama 20 baada ya mechi 25 na bado wanapambana kuepuka kushuka daraja.
Kushuka kwa KMC kunahitimisha safari ya miaka minane ya klabu hiyo katika ligi kuu. Tangu ilipopanda daraja mwaka 2018, KMC imekuwa miongoni mwa timu za kawaida katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ikishindana na baadhi ya klabu kubwa nchini.
KMC ilipanda ligi kuu baada ya kufanya vizuri katika ligi za chini na kucheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu msimu wa 2018/19. Klabu hiyo ilijijengea sifa kwa kutoa ushindani mkubwa na kuwapa wakati mgumu baadhi ya timu kongwe na zenye uzoefu mkubwa.
Moja ya mafanikio makubwa katika historia ya klabu hiyo yalikuja msimu wa 2019/20 ilipofanikiwa kufuzu kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup), ikiwa ni mara yao ya kwanza na ya pekee kucheza mashindano ya kimataifa ngazi ya klabu. Mafanikio hayo yalionyesha maendeleo ma-kubwa ambayo KMC ilikuwa imeyapata katika kipindi kifupi tangu kupanda ligi kuu.
Hata hivyo, msimu huu umekuwa mgumu kwa KMC kutokana na matokeo mabaya yaliyoiweka mkiani mwa msimamo wa ligi na kushindwa kujinasua kutoka eneo la kushuka daraja. Kushuka kwao kun-afunga rasmi sura ya miaka minane katika ligi kuu na kuwalazimu kuanza maandalizi ya maisha mapya katika Championship msimu ujao.
Sasa KMC italazimika kujipanga upya kwa lengo la kurejea haraka katika Ligi Kuu Tanzania Bara.