Kiungo Al Ahly afanyiwa upasuaji wa bega

WAKATI kiungo Alou Dieng akirejea tena uwanjani baada ya kuwa nje kwa majeruhi na kukosa mechi sita, kiungo mwingine wa Al Ahly, Emam Ashour aliyeumia juzi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa akiwa na timu ya taifa ya Misri amefanyiwa upasuaji wa bega na atakuwa nje ya muda mrefu.

Ashour aliumia kwenye pambano hilo la kimataifa la michuano maalumu ya Fifa Series dhidi ya New Zealand katika dakika ya 24 na awali ilielezwa inasubiriwa taarifa za kitabibu kujua jeraha la bega na leo klabu hiyo imetoa taarifa kwamba kiungo huyo amefanyiwa upasuaji.

Katika taarifa iliyotolewa na Ahly, imeeleza Emam amefanyiwa upasuaji na sasa yupo chini ya uangalizi wa daktari wa viungo wa timu hiyo kwa ajili ya kumuweka sawa ili arudi mapema kwenye majukumu yake, huku akiwa na hatahati ya kucheza mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba itakakayopigwa Ijumaa ya Machi 29 kuanzia saa 3:P00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa.

Taarifa za kuumia kwa mchezaji huyo wa kikosi cha kwanza cha Al Ahly huenda nui faraja kubwa kwa Simba katika mbio za kutaka kurejea rekodi ya mwaka 1974 ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo ya Afrika.

Katika mwaka huo Simba iliondolewa na Mehalla el Kubra ya Misri kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya kika timu kushinda mechi ya nyumbani kwa bao 1-0 na tangu hapo sio Simba wala timu nyingine iliyowahi kufika hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyofahamika awali kama Klabu Bingwa.

Emam amekuwa na mchango mkubwa kwa timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa msimu huu ambapo amecheza mechi zote za Ligi ya Mabingwa na kukosekana kwake Kwa Mkapa huenda likawa ni pigo kwa watetezi hao wa taji ambao watarudiana na Simba Aprili 5 jijini Cairo, Misri.

Katika mechi nane za hatua ya awali hadi makundi ilizocheza Al Ahly, Emam ametoa asisti mbili na mchezo wa mwisho dhidi ya Yanga alicheza dakika 15.

Mbali ya mchango huo kwenye michuano ya kimataifa Emam ambaye amejiunga na Ahly Julai mwaka jana akitokea FC Midtjylland ya Denmark kwa ada ya zaidi ya Sh4 bilioni, amekuwa msaada mkubwa kwenye ligi yao ya ndani ambako ametoa asisti tano kwenye mechi nane.