Kitambi aitangazia vita Simba
KOCHA Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi amesema huu ni wakati sahihi kwao wa kuweza kufuta uteja mbele ya Simba wakati timu hizo zitakapokutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, Jumatano hii.
Timu hizo zinakutana katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi huku Namungo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi ya kwanza kwa bao 1-0, Novemba 16 mwaka jana.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kitambi alisema licha ya ugumu wa mchezo huo ila ni muda wa kuondoa unyonge mbele ya wapinzani wao kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri kila wakati wanapokutana.
"Awali malengo yetu yalikuwa ni kumaliza nafasi nne za juu lakini ukiangalia kasi ya washindani wetu na kutokuwa na matokeo mazuri imeturudisha nyuma hivyo angalau tumalize ya tano," alisema.
Kitambi aliongeza katika michezo yote iliyobaki wameanza kampeni ya kuhakikisha kila mpinzani atakayefika uwanjani mwao anakutana na wakati mgumu wa kupata ushindi ili kutimiza malengo yao.
Wakati Kitambi akizungumza hayo ila timu hiyo imekuwa wanyonge kwa Simba kila inapokutana nao kwani tangu imepanda rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020 haijawahi kushinda zaidi ya sare tu.
Katika michezo saba ya Ligi Kuu Bara ambayo Namungo imecheza na Simba tangu msimu huo imepoteza mitano na kupata sare miwili tu na imefungwa jumla ya mabao 14 huku wao wakifunga matano tu.
Mchezo huu ambao utapigwa Mei 3 unarudisha kumbukumbu ya mechi baina ya timu hizi uliopigwa pia Mei 3, mwaka jana wakati miamba hii ilipokutana kwenye Uwanja wa Ilulu na kufungana mabao 2-2.
Katika mchezo huo mabao ya wenyeji Namungo yalifungwa na Jacob Masawe na Obrey Chirwa huku kwa upande wa Simba yakifungwa na beki wa kulia, Shomari Kapombe pamoja na mshambuliaji Kibu Denis.
Kwenye michezo 26 iliyocheza timu hiyo imeshinda 10, sare mitano na kupoteza 11 ikiwa nafasi ya sita na pointi 35.