Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIPRETCHE TCHE: Umemzoea uwanjani, hebu mchungulie nyumbani

Muktasari:

Nguvu, akili na mashuti ndivyo vimemfanya ndani ya miaka mitatu aliyocheza mpira wa Tanzania kufikia malengo

HAPA Tanzania hakuna asiyefahamu makali ya Muivory Coast, Kipre Tchetche anapokuwa uwanjani.

Nguvu, akili na mashuti ndivyo vimemfanya ndani ya miaka mitatu aliyocheza mpira wa Tanzania kufikia malengo.

Kutokana na mafanikio yake uwanjani, Mwanaspoti limetinga nyumbani kwake ili kufahamu anaishije nje ya uwanja. Hiyo inamaanisha uhalisia wa maisha yake anapokuwa hajihusishi kabisa na mpira.

Nyumbani kwake

Tchetche anaishi katika nyumba maalumu aliyokabidhiwa na mabosi wake wa Azam FC. Nyumba hiyo ipo maeneo ya Mtoni Kijichi, jijini Dar es Salaam.

Mazingira ya eneo la nyumba hiyo ni ya utulivu, pia nyumba nyingine zilizojengwa katika mtaa huo nyingi ni za kifahari. Eneo kubwa lipo wazi hivyo kuruhusu upepe mzuri, pia wenyeji wa maeneo hayo ni watu wanaojiweza kifedha.

Nyumba imezungukwa na uzio ambao unafanya nyota huyo asionekane na wapita njia wakati akifanya mambo yake nyumbani.

Mwanaspoti: Hodi!

Tchetche: Karibu!

Mwanaspoti: Nimefurahi kufahamu mahali unapoishi, hivi kwa nini ulichagua kuishi katika nyumba hii?

Tchetche: Sio mimi niliyechagua kuishi hapa, bali uongozi wa timu yangu ndiyo ulinikabidhi hapa.

Mazingira ya hapa ni mazuri na nafurahia kuishi katika nyumba hii kwa sababu ni kubwa na inajitosheleza kwa kitu ninachokihitaji.

Mwanaspoti: Hii ni nyumba ya ngapi unakaa tangu ulipokuja Tanzania?

Tchetche: Hii ni nyumba ya tatu lakini zote nilizokaa zipo katika eneo hili hili la Kijichi.

Nyumba ya kwanza ni ile niliyofikia katika eneo hili, pale nilikaa kwa kipindi kifupi kwa ajili ya kuandaliwa nyumba ya kudumu.

Nyumba ya pili ndiyo niliyotakiwa kuishi baada ya ile ya awali, ilikuwa kubwa na kila kitu, lakini kutokana na mahitaji na wachezaji kuongezeka, nikahamishiwa kwenye nyumba hii ya tatu.

Ninavyoona, hii ni nzuri zaidi ni kubwa ina kila kitu. Naweza kufanya chochote kulingana na mahitaji yangu.

Anaishi na nani?

Mwanaspoti: Unaishi na nani?

Tchetche: Hapa naishi na Bolou (Ni pacha wake, naye ni mchezaji wa Azam), wakati mwingine, mchumba wangu, Gauro Prisca (Naye ni Muivory Coast) anapokuja huwa anaishi hapa.

Mwanaspoti: Kumbe una mchumba, nini kilikuvutia hata ukachagua kuishi na mchumba huyo?

Tchetche: Ni mchumba, lakini ni sawa na mke wangu, kila kitu tunashirikiana. Nilimpenda kwa sababu niliona tunaendana, tunasikilizana pia nafikiri ni Mungu tu ndiye alituunganisha, yeye alikuwa ‘single’ na mimi nilikuwa ‘single’ ikawa hivyo.

Mwanaspoti: Ulikutana naye katika mazingira gani?

Tchetche: Alikuja maeneo ya nyumbani kwetu kumtembelea rafiki yake, nikampenda naye akanipenda.

Tunafurahia uhusiano wetu, ingawa katika maisha ya kawaida, mara nyingine kutoelewana huwa inatokea.

Mwanaspoti: Una watoto? Na unataka kuwa na wangapi?

Tchetche: Ndiyo, nina watoto wawili, Astride (4) na Grace (2). Lakini mpango wangu ni kuwa na watoto watatu tu.

Maisha ya kawaida

Mwanaspoti: Mambo gani huwa ni muhimu katika maisha yako?

Tchetche: Soka ndiyo maisha yangu, ndiyo muhimu kwangu.

Mwanaspoti: Unapokuwa nyumbani unapendelea kufanya nini?

Tchetche: Napenda kusikiliza muziki, kuangalia televisheni na kucheza gemu ‘Play station’).

Katika televisheni, napenda kuangalia zaidi mpira, hapa tuna ving’amuzi vyote DStv, Azam TV ni uamuzi wangu tu.

Kwenye muziki, huwa nasikiliza wa kwetu Ivory Coast, nimekuja na CD nyingi ingawa mara chache nasikiliza wa hapa. Kwa Tanzania mwanamuziki Dimaond Platnumz ndiye msanii ninayempenda zaidi.

Mwanaspoti: Huwa unapika mwenyewe au unaye mpishi?

Tchetche: Hakuna mpishi. Napika mwenyewe na mara nyingine ni zamu ya Bolou. Huwa tunapika chakula tofauti lakini chakula ninachofurahia kukiandaa ni tambi na samaki kwa sababu ndiyo napenda kukila.

Mwanaspoti: Ni sehemu gani ya nyumba unayoipenda?

Tchetche: Napenda zaidi hapa sebuleni kwa sababu ndipo panapochukua muda wangu mwingi. Nafanya mambo mengi nikiwa hapa.

Mwanaspoti: Ni sehemu gani ya nje ya nyumba yako unapendelea kukaa?

Tchetche: Huwa napenda kukaa mbele ya nyumba, nje ya geti. Hapo ni kwa ajili ya kupata hewa safi na kuangalia mandhari ya nje.

Ndipo ninapopata muda wa kuwajua pia majirani wanaoishi eneo hili.

Mwanaspoti: Nani alichangia katika uchezaji wako?

Tchetche: Ni baba yangu. Baba yangu alikuwa anacheza mpira hapo zamani lakini haukuwa wa kiwango cha kimataifa.

Mwanaspoti: Mchezaji gani anakuvutia nje ya nchi?

Tchetche: Navutiwa na Mreno Cristiano Ronaldo kwa sababu ni mpambanaji. Ni mchezaji mwenye malengo na asiyekata tamaa.

Mwanaspoti: Familia yako ni ipi?

Tchetche: Familia yangu ni Kipre kutoka Issia, Daloa, Ivory Coast. Katika familia yangu, tumezaliwa sita, mimi na Bolou ni uzao wa nne.

Wa kwanza ni Oscar, wa pili ni Carien, watatu ni Josiah, wanne ni mimi na Bolou na wa sita ni Andreas.

Mwanaspoti: Kwa nini ulichagua kuja Tanzania na umefanikiwa?

Tchetche: Ni kwa sababu ya kutafuta changamoto, hata hivyo, nimefanikiwa na nimejifunza mambo mengi ambayo yatanisaidia hata hapo baadaye.

Nafikiri nimefanikiwa, kwani nilikuwa mchezaji bora na mfungaji bora, ingawa malengo yangu ya sasa ni kutoka kwenda kucheza mpira wa ushindani zaidi Ulaya.

Mwanaspoti: Tanzania una rafiki? Hapo Azam ni mchezaji gani rafiki yako?

Tchetche: Watanzania wote ni rafiki zangu, lakini ninaye mmoja anaitwa, Herry ndiyo tunashirikiana kwa mambo mengi. Na wachezaji wote pia ni rafiki zangu ingawa mara nyingi nakuwa na Bolou kwa sababu tunaishi pamoja na kufanya mambo mengi pamoja.