Kipanga yapigishwa kwata, KMKM ikibanwa

Muktasari:
- Mafunzo ilipata ushindi huo iliyoipa pointi tatu muhimu katika mechi iliyopigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja.
MAFUNZO imerejea katika Ligi Kuu Zanzibar ( ZPL) kwa kishindo baada ya kuinyoosha Kipanga kwa bao 1-0, huku KMKM ikibanwa na Malindi kwa kutoka suluhu, ikiwa ni mfululizo wa mechi za ligi hiyo.
Mafunzo ilipata ushindi huo iliyoipa pointi tatu muhimu katika mechi iliyopigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja.
Ushindi huo uliotokana na bao la dakika 44 la Ibrahim Ndamba umeifanya Mafunzo kuganda nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 44 ikilingana na Mlandege japo zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa nyuma ya vinara, Mwembe Makumbi yenye alama 45, kila moja ikicheza mechi 23.
Huo ni ushindi wa inashikilia nafasi ya tatu 13 kwa Mafunzo.
Licha ya kufungwa, lakini Kipanga ilionyesha ushindani katika mechi hiyo, ila iliangushwa na umakini mdogo wa washambuliaji wa timu hiyo na kujikuta dakika 90 zikiisha ikilala kwa bao hilo.
Katika mechi nyingine ya Ligi hiyo uliopigwa pia Mao A, KMKM na Malindi zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu.
Kocha wa Malindi, Suleiman Mo amesema timu hiyo imecheza vizuri japo ilishindwa kutoka na ushindi mbele ya maafande wa majini, huku Ame Msimu wa KMKM amesema kabla ya mchezo huo walikuwa na matumaini ya kutoka na ushindi ili kusogeza nafasi, licha ya yote watamaliza katika msimamo hao wakiwa katika kundi la 10 bora.
Ligi hiyo itaendelea kesho itawakutanisha New City na JKU Mao A, na mchezo huo utahitimisha mzunguko wa 23 ya ligi hiyo.
Mechi ya kesho ndio itakayotoa hatma ya New City kubaki Mjini au kubeba mizigo yao kurudi kwao kwani ikipoteza itaungana na Tekeleza na Inter Zanzibar zilizoshuka daraja mapema.