Kina Enekia waanza pale walipoishia Mexico

Muktasari:
- Nyota hao ni Julietha Singano anayeichezea Juarez na Enekia Lunyamila wa Mazaltan wakiwa ni Wabongo pekee wanaocheza Ligi hiyo kubwa ya Amerika ya Kaskazini.
WATANZANIA wawili wanaokipiga Ligi ya Wanawake ya Mexico kila mmoja ameanza msimu mpya kama walivyomaliza msimu uliopita.
Nyota hao ni Julietha Singano anayeichezea Juarez na Enekia Lunyamila wa Mazaltan wakiwa ni Wabongo pekee wanaocheza Ligi hiyo kubwa ya Amerika ya Kaskazini.
Msimu uliopita chama la Lunyamila, lilimaliza katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi likikusanya pointi 10, ushindi mechi tatu, sare moja na kupoteza 13.
Juarez anayeichezea Singano ilimaliza ndani ya 5-bora ushindi mechi 10, sare mbili na kupoteza tano na kujizolea pointi 32.
Ni kama wanaendelea pale walipoishia kwani ukiwa msimu mpya ambao tayari zimechezwa raundi mbili, Juarez imecheza mchezo mmoja na kushinda mabao 3-0 dhidi ya Puebla.
Kwa upande wa Mazaltan mambo yameendelea kuwa mabaya kwao ikichezea vichapo michezo miwili dhidi ya Toluca 5-0 na Monterrey 7-0.
Hata hivyo, nyota hao wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ wameendelea kuaminiwa ndani ya kikosi hicho wakicheza kwa dakika zote.