Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichozipunguza makali JKT, ABC, Srelio BDL

Muktasari:

  • Ligi hiyo ambayo inachezwa kwa mzunguko mmoja imekuwa na mvuto na ushindani unaochangiwa na uwepo wa bonasi zinazotolewa na wadhamini kwa wachezaji na timu zinazoshinda.

LIGI ya Kikapu Dar es Salaam (BDL) inazidi kushika kasi huku timu kongwe zikijikuta zikisuasua zikiwamo JKT, ABC na Srelio.

Ligi hiyo ambayo inachezwa kwa mzunguko mmoja imekuwa na mvuto na ushindani unaochangiwa na uwepo wa bonasi zinazotolewa na wadhamini kwa wachezaji na timu zinazoshinda.

Ushindani huo ndiyo umezifanya timu hizo zilizocheza robo fainali mwaka jana, kukutana na upinzani mkubwa na kushindwa kuonyesha makali yao katika kufukuzia nafasi ya kucheza nane bora.

JKT iliyofungwa michezo 3-0 na Dar City katika fainali mwaka jana , ilipata pigo baada ya kuondokewa na nyota wake Ronaldi Kisobwe, Baraka  Sabibi na Jordan Manang waliotimukia Veins BC, huku sababu nyingine ya kuchemka mwaka huu ikitajwa ni majeraha ya wachezaji akiwamo Baraka Sadiki.

Katika michezo yake, ilifungwa na Stein Warriors kwa pointi 70-52, Pazi pointi 79-61, ABC pointi 70-68, iliifunga Vein BC pointi 57-56 na DB Oratory pointi 69-61.

Mmmoja wa viongozi wa timu hiyo, Chares Makene alisema licha ya changamoto hizo, timu hiyo itakaa vizuri katika mechi zinazokuja.

“Kwa sasa tunaboresha timu, baada ya kuwaibua wachezaji kutoka kambi ya JKT naamini wakija kuzoea mikiki mikiki ya ligi watakuja kushangaza,” alisema Makene.

Nyota wanaounda kikosi hicho ni pamoja na Rajabu Mbonde, Prudensia Shija, Elias Paul, George Petar, January Wilbard, Daudi Songo, Anthony Gosbert, Ndalawa Juma na Dotto Zephania na Omari Ndula.

Wengine ni Saidy Shabani, Juma Hamisi,Mohamed Kassim. Ezra Elias, Mussa Chacha na kati yao, Ndula, Chacha, Zephania na Mbonde ndio wazoefu wa ligi.

Kwa upande wa ABC, licha ya kushinda baadhi ya mechi, inaongoza kuwa na wachezaji ambao ni majeruhi na huku baadhi yao wakiwa katika majukumu mengine ya kikazi na ndiyo inatajwa sababu ya kufanya vibaya mwaka huu.

Katika mechi zake, iliifunga JKT kwa pointi 70-68, Ukonga Kings pointi 71-62, ilifungwa na  Vijana 'City Bulls' pointi 61-51 na Stein Warriors pointi 91-43.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Filbert Mwaipungu  aliwataja wachezaji wanaocheza wakiwa ni majeruhi ni  Elias Nshishi, Enerico Maengela na Moses Zacharia, huku walioko katika ya kikazi nje ya Dar es Salaam ni Alinani Msongole,  Yekonia Mpambije, Bundala Denlison na Stanley Denis.

Kwa upande wa Srelio haijaonyesha makali yake baada ya kushindwa kusajili nyota wao wa kimataifa waliotoa mchango mkubwa katika ligi  ya mwaka jana.

Mchezaji mwandamizi wa timu hiyo, Mussa Mwakalobo alitaja wachezaji hao kuwa  ni  Daniel Kola aliyetimkia Stein Warriors , Spoican Ngoma (Zambia), Lerry Rostand (Gabon).


LIGI KUENDELEA JUMAMOSI

Kamishina wa Ufundi na Mashindano, Shabani Mahobonya alisema ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kesho (Jumamosi) kwenye Uwanja wa Donbosco Upanga na mechi ya kwanza itazikutanisha Kurasini Divas dhidi ya Vijana Queens, ikifuatiwa na City Queens dhidi ya Twalipo Qeens, huku Mlimani BC dhidi ya ABC na ya mwisho ni Veins na Ukonga Kings.

Veins BC na Ukonga Kings zinatarajiwa kuonyesha mechi kali na yenye ushindani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili.

Kocha wa Ukonga, Denis Lipiki alisema anatarajia kushusha kikosi chake chote akiwepo Mustapha Haji, Ismail Saad, Magige Thomas na Bahati Jacobu.