Kikosi cha Pep Guardiola kiko tayari kwa lolote
Muktasari:
- Februari ni mwezi wa Bayern kuangazia mambo, mtazamo wa kiwango kizuri cha uchezaji cha Januari si tu ulimaanisha ushindi na tofauti kubwa ya pointi katika ligi ya Bundesliga, pia uliwawezesha kubadili mtazamo wao na kuanza kuifikiria Ligi ya Mabingwa jambo ambalo Pep alikuwa akitaka kuachana nalo hadi hapo watakapotwaa taji la Bundesliga.
KATIKA toleo lililopita kwenye Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau alizungumzia hamasa iliyoanza kuonekana katika timu huku wachezaji wakiwa na shauku ya kupata mafanikio ya mataji matatu waliyoyapata kabla ya Kocha Pep Guardiola kuanza kuinoa timu hiyo. Endelea…
Februari ni mwezi wa Bayern kuangazia mambo, mtazamo wa kiwango kizuri cha uchezaji cha Januari si tu ulimaanisha ushindi na tofauti kubwa ya pointi katika ligi ya Bundesliga, pia uliwawezesha kubadili mtazamo wao na kuanza kuifikiria Ligi ya Mabingwa jambo ambalo Pep alikuwa akitaka kuachana nalo hadi hapo watakapotwaa taji la Bundesliga.
Hata hivyo, hilo ni jambo lisiloepukika na wachezaji hadi hapo akili zao zikawa huko, walipambana katika mazoezi yao huku wakidhihirisha shauku waliyokuwa nayo, tayari walishaonja utamu wa taji la Ligi ya Mabingwa na hawakutaka kuona utamu huo ukiwaponyoka mikononi mwao.
Unapowaangalia wachezaji mazoezini wakati wakicheza kwa staili ya kujipanga na kutumia maeneo yao, unakuwa kama vile unamwangalia Thiago akionyesha umakini katika uwezo wake wa kumiliki mpira, Thiago ana sifa ya kufungua vyumba kila wakati mpira unapokuwa kwenye himaya yake.
Hii ni aina ya mazoezi ambayo hufanywa katika eneo la ukubwa wa mita 20 kwa 12 na wachezaji saba hucheza dhidi ya saba pamoja na wengine watano ambao huingia kutoa msaada.
Ni wateule wachache tu, Thiago, Lahm, Schweinsteiger na Kroos ambao wanaoruhusiwa kuugusa mpira na kuuchezea lakini kwa wengine wote wanachoruhusiwa ni kuugusa mara moja. Hapo hapo, Pep pia hachoki kurekebisha mambo bila kujali kama ni Kroos, Robben au Schweinsteiger.
“Ni pa, pa pa, pasi zinakwenda kwa uhakika, angalia, geuzia upande mwingine, tulia na mpira, chukua eneo sahihi,” anasema Pep.
Timu inaonyesha hali ya usalama, inaonekana, Bayern kwa mara ya kwanza tangu Pep aanze kuiongoza timu hiyo imefikia hatua isiyofikika ambako wanajiona wakiwa katika hali ya kukabiliana na mazingira yote mabaya.
Pep amewapa nguvu ya usalama wao uwanjani inayowafanya wawe na amani wana uwezo wa kushinda kila kitu. Kumbukumbu za maisha ya Barcelona zikaanza kurudi kwa kasi, wakati ule Barca ilipojiona kuwa ni aina ya timu isiyoshindwa na chochote.
Mwishoni mwa mazoezi yao ya mwisho kabla ya kuivaa Arsenal jijini London katika mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora, nilimuuliza Thiago Alcantara kuhusu hamasa waliyokuwa nayo.
“Hakika upo sahihi,” anasema Thiago, “Nilikuwa nafikiria kuhusu hilo jana usiku na ndicho ninachokiona hali ya kuwapo usalama na mambo kuwa kwenye mstari, timu inajiona katika amani na ina uwezo wa kufanya lolote, nilikuwa na fikra hizo hizo majira ya kiangazi mwaka jana wakati wa fainali za Ulaya kwa vijana chini ya miaka 21.
“Timu ya Hispania tuliamini lazima tushinde, hatukuwa na mpinzani, kwamba timu pekee ambayo ilikuwa na uwezo wa kutufunga ni sisi wenyewe. Na kweli tulishinda,” anasema Thiago akifafanua kuhusu mwenendo wa Bayern chini ya Pep.
Kuna mtu mmoja aliyebaki wa kuizungumzia Bayern na mazingira inayopitia, mtu ambaye huwa hapuuzi hali ya kuwapo presha, mtu ambaye hana tabia ya kuchukulia mambo poa, mtu huyo ni Matthias Sammer, mkurugenzi wa michezo wa klabu.
“Tuko katika kiwango kizuri, tuko imara, sisi ni Bayern, tunatakiwa kujitoa kwa nguvu zote katika kila mazoezi na katika kila mechi, hiyo ndiyo njia pekee ya kupata mafanikio makubwa, kufikia kiwango cha juu ambacho ni kwa ajili ya klabu washindi wa kweli.
“Hii ni fursa ya kihistoria, sisi ni Bayern na tunahitaji kufanya kila kitu katika kuitumia fursa hii, hatutakiwi kusimama kwa wakati huu.
Itaendelea Jumanne ijayo…