Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kidiaba: Nyota TP Mazembe aliyeukwaa uwaziri

Muktasari:

  • Bila shaka Tshisekedi hakufanya kosa kumchagua Kidiaba kuwa waziri wa michezo katika Serikali yake kwa kuwa anatambua ni mtu wa aina gani katika sekta hiyo.

Dar es Salaam. Robert Kidiaba ni jina maarufu katika soka la Afrika na Ulaya, akiwa kipa namba moja wa timu ya TP Mazembe Englebert ya DR Congo.

Mbali na kucheza kwa mafamikio makubwa katika ngazi ya klabu, nguli huyo alikuwa mhimili wa timu ya Taifa ya DR Congo kwa muda mrefu.

Pamoja na kucheza soka kwa kiwango bora, Kidiaba (43) ni maarufu zaidi kwa staili yake ya kipekee ya aina ya kushangalia.

Staili yake ya kushangilia huku akiwa amesuka rasta sehemu ndogo tu ya kichwa chake, ilimtambulisha rasmi Kidiaba katika medani ya soka duniani.

Haikuwa ajabu kwa idadi kubwa ya vijana kuiga mtindo wa kusuka nywele au kucheza kwa kurukaruka pindi timu inapofunga bao.

Kwasasa nguli huyo si Kidiaba tuliyemzoea uwanjani, nyota huyo ameula baada ya kuingia katika baraza la mawaziri chini ya Rais Felix Tshisekedi.

Baada ya kushinda ubunge katika Jimbo la Katanga, nyota huyo sasa ni Waziri wa Michezo wa DR Congo, eneo ambalo ana uzoefu wa kutosha.

Bila shaka Tshisekedi hakufanya kosa kumchagua Kidiaba kuwa waziri wa michezo katika Serikali yake kwa kuwa anatambua ni mtu wa aina gani katika sekta hiyo.

Baada ya kucheza TP Mazembe kwa miaka 16 kabla ya kustaafu mwaka 2016 na kuteuliwa kocha wa makipa wa TP Mazembe, mchango wa Kidiaba katika soka ulionekana kuwavutia wanasiasa nchini humo.

Kidiaba anaendeleza maisha katika kazi yake ya siasa ikiwa ni miezi michache tangu aliposhinda Ubunge wa Jimbo la Katanga jijini Lubumbashi.

Kidiaba aliyezaliwa Februari Mosi 1976, alianza kucheza soka katika klabu ya AS Saint-Luc mwaka 2001 ambako alicheza kwa mwaka mmoja kabla ya kutua TP Mazembe 2002.

Kidiaba hakuhitaji muda mrefu kuanza kucheza katika kikosi cha kwanza TP Mazembe, alivyotua tu na kuanza kupata nafasi ndipo ulipokuwa mwanzo wake wa kucheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho.

Nyota huyo aliibeba TP Mazembe kushinda mataji mengi ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, akiwa na wachezaji wa Tanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Katika miaka ambayo alicheza kwa miamba hiyo ya soka ya DR Congo na Afrika,  ametwaa mataji tisa ya Ligi Kuu nchini humo miaka ya 2006, 2007, 2009, 2011, 2012, 2013, 2014, 2016 na 2017.

TP Mazembe imetwaa mara tatu Kombe la FA na  awamu zote hizo, ilikuwa na Kidiaba golini miaka ya  2013, 2014 na  2016.

Upande wa mshindano ya kimataifa, nyuma ya mafanikio ya TP Mazembe alikuwepo Kidiaba ambaye alichangia timu hiyo kushinda mara tatu mataji ya Ligi ya Mabingwa Afrika miaka ya 2009, 2010 na 2015.

Kidiaba aliikuta TP Mazembe ikiwa na mataji mawili tu iliyotwaa miaka ya 1967 na 1968 kipindi hicho Ligi hiyo ya Mabingwa Afrika ikitwaa kombe la washindi.

Kipa huyo alifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa ya mwaka 2015 ambapo mbali na kuiwezesha TP Mazembe kutwaa ubingwa, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakiwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika wa mwaka kwa wachezaji ndani akiwa na Samatta.

Samatta katika ubora wake aliweka wavuni mabao saba katika kikosi cha TP Mazembe yaliyomzidi kete Kidiaba na kutwaa tuzo hiyo.

Kidiaba mwaka huo, alianza kuiongoza TP Mazembe akiwa golini kwenye michezo ya makundi ambapo walikuwa Kundi A na vigogo wengine  Al-Hilal, Moghreb Tetouan na Smouha katika michezo yote  ya makundi alifungwa bao moja tu.

Katika michezo miwili ya nusu fainali dhidi ya  Al-Merrikh ya Sudan kwa maana ya nyumbani na ugenini alifungwa jumla ya mabao mawili na walisonga mbele kwa jumla ya mabao  4-2 na kwenda kwenye fainali ambapo walicheza na USM Alger.

Kidiaba alifungwa bao moja katika michezo yote miwili ya fainali ambapo TP Mazembe ilitwaa ubingwa kwa jumla ya mabao 4-1 hivyo msimu huo, hivyo alifungwa jumla ya mabao manne.

Kumbukumbu nyingine itakayobaki kwa Kidiaba ni kuwa sehemu ya kikosi cha TP Mazembe kilichocheza  Fainali ya Ligi ya Mabingwa Duniani mwaka 2010 dhidi ya Inter Milan ya Italia na kufungwa mabao 3-0.