Kazi imeanza! Kamusoko, Okwi waaga mapemaa
Muktasari:
- Kamusoko ameandika kuwa amewakumbuka rafiki zake ambao ni wachezaji wenzake na kuweka wazi kuwa, walikuwa ni zaidi ya ndugu kwake.
SIKU mbili tu kabla ya Kocha Mwinyi Zahera kutembeza panga kla kuwatema nyota waliopo Yanga kwa sasa, kiungo mkongwe, Thabani Kamusoko ameamua kujichomoa mwenyewe kimyakimya, huku akiungana na Emmanuel Okwi wa Simba kuaga mapema.
Okwi kupitia akaunti yake ya Instagramu aliandika mchana ‘Kwaheri ni neno la simanzi mno’ kuonyesha anajisikia vibaya kuwaaga mashabiki wa klabu hiyo kuhitimisha kazi zake alizokuwa akiifanya Msimbazi tangu arejeshwe misimu miwili iliyopita na kuifungia mabao 35 katika Ligi Kuu mbali na mechi nyingine mbalimbali.
Lakini, Okwi akiaga hivyo kimtindo, naye Mzimbabwe Kamusoko aliyetua Yanga mwaka 2015 amemaliza mkataba na Yanga inayojiandaa kuvaana na Azam kesho Jumanne kufunga pazia la msimu huu, akiwa ameifungia bao moja akitumia mtandao wa instagramu naye aliaga kuonyesha hatakuwepo Yanga msimu ujao.
Kamusoko ameandika kuwa amewakumbuka rafiki zake ambao ni wachezaji wenzake na kuweka wazi kuwa, walikuwa ni zaidi ya ndugu kwake.
“Nimewakumbuka sina neno lingine zaidi la kuzungumza nimewakumbuka sana nikisema rafiki ni neno dogo sana kwenu nyinyi mlikuwa ni zaidi ya rafiki kwangu,” aliandika Kamusoko.
Mwanaspoti lilimtafuta Kamusoko aliyeitwa kikosi cha awali cha timu ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Mighty Warriors’ na kusema bado ni mchezaji wa Yanga hadi mkataba wake utakapomalizika huku akifichua ataukosa mchezo wa kesho dhidi ya Azam.
“Ni kweli namaliza mkataba na Yanga msimu huu na hakuna mazungumzo yoyote niliyoanza kufanya na uongozi, lakini sina maana kwamba kuandika hivyo ndio naondoka Yanga nitaondoka nikimaliza mkataba, nimeandika hivyo wa vile nipo mbali na wenzangu muda mrefu,” alisema na kuongeza;
“Pia kuna maisha nje ya Yanga ni vizuri kuwakumbuka rafiki zangu ambao, nimeishi nao vizuri katika klabu hiyo ambayo naweza kusema ndio timu ya kwanza kunipa taji la ligi tangu nimeasha kucheza soka la ushindani naipenda sana.”
Kamusoko alifichua kwamba, maisha aliyoishi ndani ya Yanga yamemfunza mengi akiandikisha historia mpya ambayo alikuwa hajawahi kupata tangu ameanza kushiriki ligi ya ushindani.