Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KARIAKOO DERBY : Yanga vs Simba usibeti hii mechi ni ya mtego

Muktasari:

Hapa chini ni dondoo fupi za kuelekea pambano hilo linalochezwa Jumapili ya Machi 8, ikiwa ni Siku ya Wanawake Duniani.

HUKO mtaani kwa sasa mashabiki wa Simba na Yanga presha zipo juu. Hii ni kwa sababu ile ‘dabi’ ya timu zao inapigwa wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa. Pambano la Jumapili hii litakuwa la 104 kwa timu hizo katika Ligi ya Bara tangu 1965. Licha ya presha za mashabiki, lakini kila timu kwa sasa ina mzuka mwingi kwa ajili ya mchezo huo. Kila moja inaamini lazima itakate Taifa. Yanga wanatambia fundi wao wa mpira, Bernard Morrison na Haruna Niyonzima na wengine, huku Msimbazi wakitambia silaha kali kutoka Msumbiji, Luis Jose Miquissone na vifaa vingine matata.

Hapa chini ni dondoo fupi za kuelekea pambano hilo linalochezwa Jumapili ya Machi 8, ikiwa ni Siku ya Wanawake Duniani.

HAKUNA MBABE

Kama hujui ni kwamba pambano la Jumapili ndani ya Machi ni la nane kwa vigogo hao wa soka Tanzania.

Kabla ya hapo timu hizo zilishakutana mara saba ndani ya mwezi huu, lakini hakuna mbabe anayeweza kumcheka mwenzake, kwani kila moja imewahi kupata ushindi mara moja.

Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kushinda ndani ya mwezi huo kwa kuitungua Simba kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Machi 27, 1993. Katika mchezo huo, Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa Said Mwamba Kizota katika dakika za 47 na 57, huku la Simba likitupiwa na Edward Chumila katika dakika ya 75.

Simba ilikuja kujibu mapigo tarehe kama ya mchezo wa wikiendi hii, yaani Machi 8, ila mwaka 2015 kwa bao tamu la shuti la mbali lililowalaza Yanga mapema la Emmanuel Okwi katika dakika ya 52.

Katika mechi zao saba za awali za Machi, timu hizo zimetoka sare tano na kila moja kufunga jumla ya mabao matano.

Sare hizo tano ni pamoja na ile ya 1-1 ya mchezo uliopigwa Machi 10, 1984, kisha 1-1 ya Machi 15, 1986, 0-0 ya Machi 18, 1995, pia 0-0 ya Machi 26, 2006 na ile ya 1-1 ya Machi 11, 2011.

JUMAPILI YA SIMBA

Inawezekana ni imani tu, lakini ukweli ni kwamba Simba imekuwa na kismati na Jumapili, kwani katika mechi zao 32 za awali walizokutana kwenye siku hiyo wameitingisha Yanga kinoma.

Rekodi zinaonyesha kwenye siku hiyo Simba imeshinda mechi nane dhidi ya tano za watani wao, huku 19 zikiisha kwa sare.

Katika mechi hizo za awali 32, wababe hao wametengeneza jumla ya mabao 61, huku Simba ikifunga 34 dhidi ya 27 ya vijana wa Jangwani ambao Jumapili hii wao ni wenyeji.

Katika Jumapili ambazo Simba ilipata ushindi katika mechi nane, Wekundu wa Msimbazi, wana rekodi ya kuitia aibu Yanga kwa kipigo kizito kinachoendelea kuwatesa mpaka leo hii.

Kwa wanaokumbuka ni Jumapili ya Mei 6, 2012 ndipo Simba ilipoifumua Yanga kwa mabao 5-0 wakati wakifunga msimu wa 2011-2012 na Wekundu wakiwa wamejihakikishia kubeba taji la 18.

Pia Simba iliwahi kuifumua Yanga mabao 3-1 katika mechi ya Okt 7, 1979 sambamba na kuiduwaza Yanga katika sare ya maajabu ya 3-3 wakitoka mapumziko wakiwa nyuma ya mabao 3-0. Mabao ya Simba yaliwekwa kimiani na Betram Mombeki katika dakika ya 55, Joseph Owino (dk 57) na Gilbert Kazze (dk 83), huku yale ya Yanga yakifungwa na Mrisho Ngassa dk 14 na Hamis Kiiza aliyetupia mawili katika dakika za 35 na 45.

HATA YANGA WAMO

Licha ya kusadikika Jumapili huwa ni ya Simba kama ilivyo kwa Jumamosi inavyotajwa kuwa ni zali kwa Yanga, lakini wikiendi hii lolote linaweza kutokea.

Yanga licha ya kuwa na wakati mgumu kwenye mechi za Jumapili lakini hata wao nao wamo, kwani rekodi zinaonyesha katika mechi zao tano walizoshinda ndani ya siku huu dhidi ya Simba, Vijana wa Jangwani hawajawahi kuruhusu wavu wao kuguswa kabisa.

Ndio, kwani ilishinda mechi ya kwanza ndani ya Jumapili dhidi ya Simba kwa bao 1-0 mnamo Juni 18, 1972, ikashinda tena 1-0 katika mechi ya April 12, 1992 na kuifumua Simba 2-0 mechi iliyopigwa Feb 25, 1996.

Yanga wakadhihirisha kuwa wakiamua kushinda Jumapili, basi lazima Mnyama apigwe kavu, kwani Agosti 29, 1999 waliishinda pia 2-0 kabla ya kushinda mechi yao ya mwisho ya Jumapili Okt 26, 2008 kwa bao 1-0. Kama umesahau bao hilo pekee lililofungwa na Ben Mwalala ndilo lililovunja minyororo ya unyonge wa Yanga mbele ya Simba iliyocheza miaka nane mfululizo bila ushindi.

Pia ni Yanga hao hao waliowagomea watani wao na kumaliza mechi 19 kwa kutoka sare tofauti wakivuna jumla ya mabao 17 kwenye mechi hizo.

Je, ni Simba itakayoendeleza ubabe ndani ya wikiendi hii ama ni Yanga itakayopindua meza kibabe safari hii au goma litaisha kwa sare kama pambano lao lililopita la msimu huu? Tusubiri tuone!