Kadi nyekundu zamponza refa

KADI mbili nyekundu alizotoa mwamuzi Gabriel Masimbazi zilimweka matatani akijikuta akiwambwa makofi na mchezaji Joseph Isco aliyekuwa akiichezea Dortmund wakati wa mechi baina yao dhidi ya Bilo FC katika michuano ya Ilemela DC Cup.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Sabasaba jijini Mwanza, ulikuwa wa kumpata mshindi wa tatu na tukio hilo liliwaacha mashabiki midomo wazi.
Ilikuwa hivi, mwamuzi Masimpazi alianza kumwonesha kadi nyekundu kocha wa Bilo FC, Ibrahim Mlumba kwa kuingia eneo la kuchezea ‘Pitch’ kabla ya mambo kumbadilikia dakika ya 85 alipotoa kadi tena kwa mchezaji Isco wa Dortmund.
Isco baada ya kuoneshwa kadi hiyo nyekundu alionekana kutoridhishwa wala kufurahishwa na adhabu hiyo na kumvaa refa huyo kwa kumrushia ngumi kabla ya wachezaji na mashabiki kumtuliza.
Hata hivyo katika mchezo huo Dortimund iliibuka na ushindi wa mabao 3-2, huku ya washindi yakiwekwa wavuni na Elian Sndro aliyetupia mawili na Ramadhan Stopa, huku Khamis Mrisho na David Domisian wakiifungia Bilo FC.
Wakati huo huo, Bawela FC ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kuilaza Copco U20 penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Matokeo hayo yaliifanya Bawela kuondoka na zawadi ya Ng’ombe, seti moja ya jezi, huku Copco U20 wakiondoka na Mbuzi mnyama huku Dortimund na Bilo FC wakipata Jezi na mpira kila mmoja.
Jumla ya timu 16 kutoka Wilaya ya Ilemela zilishiriki michuano hiyo ambayo ililenga kuwapa nafasi vijana kuonesha vipaji vyao na kuhitimishwa juzi jijini hapa huku ikielezwa kuwa endelevu.