Julio aanza na ushindi Singida, Kayoko atembeza kadi Kirumba

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

  • Kabla ya leo, mara ya mwisho Singida Fountain Gate kupata ushindi ilikuwa ni Novemba 27, 2023 ilipoifunga Coastal Union mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Liti, Singida.

Mwanza. Unazifahamu 'Agenda 10 za Julio?' Kama huzifahamu basi tambua kwamba ni mechi 10 za kumalizia msimu ambazo Singida Fountain Gate imempa kocha wake mpya, Jamhuri Kihwelo 'Julio' na mwamba huyo ameanza na ushindi leo.

Agenda ya kwanza Julio ameimaliza kibabe kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Namungo leo Machi 16, 2024 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Julio ambaye amejiunga na timu hiyo Machi 12, mwaka huu akirithi mikoba ya Thabo Senong, ameiwezesha Singida FG kupata ushindi huo muhimu ambao ni wa kwanza kwao ndani ya muda wa zaidi ya miezi mitatu.

Mara ya mwisho Singida Fountain Gate kupata ushindi ilikuwa ni Novemba 27, 2023 ilipoifunga Coastal Union mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Liti, Singida.

Pia ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa tangu ilipohamishia mechi zake za Ligi Kuu huku ikipoteza mbili kwa kufungwa 2-0 na Mtibwa Sugar na 1-0 dhidi ya Azam FC.

Bao pekee la Singida Fountain Gate katika mchezo wa leo ambao uligubikwa na matukio ya kuvutana lilifungwa na Nicolas Gyan katika dakika ya 15 kwa shuti kali kutoka nje kidogo ya lango na kumshinda kipa, Jonathan Nahimana.

Mshambuliaji Francy Kazadi alishindwa kuiandikia timu yake bao la pili baada ya kukosa penalti kufuatia shuti lake kudakwa na kipa, Nahimana na dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa Singida Fountain Gate kuondoka na ushindi wa bao 1-0.

Mwamuzi wa mchezo huo, Ramadhan Kayoko amekuwa gumzo baada ya kutembeza kadi nyekundu kwa wachezaji wa timu zote mbili, ambapo katika dakika ya 30 aliwaonyesha kadi nyekundu ya moja kwa moja, wachezaji Erasto Nyoni (Namungo) na Thoman Ulimwengu (Singida) baada ya kutaka kupigana.

Dakika ya 87, akamuonyesha kadi nyekundu Dickson Ambundo wa Singida baada ya kumchezea madhambi beki wa Namungo, Hassan Kibailo, ambapo kadi hiyo nyekundu ilitoka na kadi mbili za njano.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Ushindi huo ambao ni wa sita msimu huu, umeifanya Singida Fountain Gate ifikishe alama 24 na kukamata nafasi ya saba ikipanda kutoka nafasi ya 11, huku Namungo ikibaki katika nafasi ya tisa na pointi 23.

Mchezo ujao, Singida Fountain Gate itaialika Yanga Aprili 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.


Akizungumzia siri ya ushindi huo, kocha wa Singida Fountain Gate, Jamhuri Kihwelo 'Julio', alisema baada ya kutua klabuni na kufanya mazoezi na wachezaji kwa siku tatu ameongeza morali, hali ya kujiamini na utayari wa kupambana kwa wachezaji kwani aliwakuta wakiwa wamekata tamaa baada ya wachezaji saba kuondoka katika dirisha dogo na kuhamia Ihefu.

Julio ameahidi mashabiki wa timu hiyo na viongozi kwamba ushindi huo siyo nguvu ya soda au kubahatisha bali utaendelea katika mechi zijazo na kuhakikisha malengo ya uongozi wa timu ya kuvuna pointi 30 katika mechi 10 yanatimia.

Kocha wa Namungo, Mwinyi Zahera amesema kikosi chake kimelazimishwa kupoteza mchezo wa leo kutokana na uamuzi wa refarii ambao umewaumiza, huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kupambana japokuwa hawakuwa na bahati.