Job, Bacca wampa presha Kocha Mamelodi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ikiwa zimebaki saa chache kabla ya mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Yanga unaotarajiwa kupigwa kesho Ijumaa jijini Pretoria, Sauzi, kocha wa wenyeji Rhulani Mokwena amewataja mabeki wa kati wa vijana wa Jangwani, Dickson Job na Ibrahim Bacca.


Timu hizo zitavaana kwenye Uwanja wa Luftus Versfeld kuanzia saa 3:00 usiku baada ya wikiendi iliyopita kushindwa kufunga katika mchezo wa kwanza uliopigwa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ambapo mabeki hao wa kati walionyesha ubora wa hali ya juu katika kuwazuia nyota wa Mamelodi.

                   
Mokwena amewataja mastaa hao wa Yanga kama sehemu ya ubora wa kikosi hicho katika eneo la ulinzi akisisitiza, amefanya uchambuzi yakinifu kuhakikisha anakuja na njia ya kuwafungua ili wapate ushindi.

                      
Kocha huyo amesema amejaribu kuangalia baadhi ya mechi mbalimbali za aina za timu kucheza kwa kuzuia zikiwamo za Ligi ya England na Afrika Kusini pamoja na kuuchambua mchezo wa kwanza baina yao uliochezwa Dar es Salaam,  ingawa anaamini Yanga inaweza kuja tofauti katika mchezo huo wa kesho.


"Ni ngumu kuifungua timu yenye kuzuia vizuri na kutoruhusu mashimo, nimeangalia namna ya kukabiliana na hili, lakini kuna muda Yanga walikuwa wakijaribu kucheza kuanzia nyuma ambapo pia walikuwa wakifanya vizuri," alisema Mokwena.


Akiizungumzia suluhu waliyopata katika mchezo wa mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam, kocha huyo amesema wachezaji wa timu hiyo ya Mamelodi watatakiwa wawe makini.


"Lakini tumeshawahi kucheza mechi za aina hii, kupata suluhu ugenini na kumalizia mechi nyumbani, tunajua namna inavyokuwa na naamini uzoefu ambao tumeupata katika mechi hizo unaweza kusaidia."


Msimu uliopita Mamelodi ilitolewa na Wydad Casablanca ya Morocco katika hatua ya nusu fainali ya michuano hii baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Morocco kumalizika kwa suluhu kisha marudiano pale Afrika Kusini ukamalizika kwa sare ya 2-2.


"Niliwaambia Yanga ni timu kubwa, ukiangalia mwaka jana walifika fainali ya Shirikisho na msimu huu wamepita katika kundi gumu, hivyo nategemea mechi ngumu lakini nipo tayari,"

amesema Mokwena aliyeiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa michuano mipya ya Ligi ya Afrika, African Football League (AFL) kwa kuifunga Wydad kwa jumla ya mabao 3-2.ss