Intaneshino

Muktasari:
Yanga walikuwa wakijigamba kwamba wao hesabu zao zipo kimataifa zaidi na hawajivunii ushindi mwembamba kama Simba inaoshinda kwenye Ligi ya ndani kupitia kwa straika wao Emmanuel Okwi na kujivuna.
USHINDI wa mabao 5-1 iliopata Yanga dhidi ya Platinum ya Zimbabwe kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho umegeuka nongwa kwa Simba.
Yanga walikuwa wakijigamba kwamba wao hesabu zao zipo kimataifa zaidi na hawajivunii ushindi mwembamba kama Simba inaoshinda kwenye Ligi ya ndani kupitia kwa straika wao Emmanuel Okwi na kujivuna.
Lakini mashabiki hao wa Yanga wakazidi kuwakera zaidi Simba kwa kuwaambia kwamba wao si saizi yao kwa vile hata Ligi Kuu Bara wameshindwa kuongoza tangu msimu huu uanze. Yanga imetumia vizuri faida ya kucheza nyumbani baada ya kuwamaliza Wazimbabwe hao ambao kwenye mitandao ya kijamii walihusisha ushindi huo wa jana Jumapili na imani za kishirikina.
Mfungaji bora wa Yanga katika michuano ya Afrika mwaka jana, Mrisho Ngassa alifunga mabao mawili, viungo Salum Telela na Haruna Niyonzima pamoja na straika Mrundi Amissi Tambwe walifunga moja kila mmoja na kupeleka kilio kikubwa kwa vijana hao kutoka wa Rais mzalendo Robert Mugabe. Walter Musoma ndiye aliyefunga bao la kufutia machozi kwa upande wa Platinum ambayo inamilikiwa na matajiri wa madini.
Matokeo hayo yameiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo kuelekea mchezo wa marudiano utakaofanyika wiki mbili zijazo huko Zimbabwe na ikiwa hivyo, itakutana na mshindi kati ya Etoile Du Sahel ya Tunisia na Benefica de Luanda ya Angola. Etoile ambayo inadaiwa Dola 300,000 na Simba za mauzo ya Okwi iliwashinda Waangola bao 1-0 wakiwa Tunisia hivyo wanakwenda machinjioni Luanda.
Yanga licha ya kuwakosa nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Andrey Coutinho ambao ni majeruhi, Niyonzima alipokea pasi nzuri ya Simon Msuva na kukosa bao la wazi katika dakika ya 22 baada ya shuti lake kwenda nje kidogo ya lango.
Telela alitumia ufundi alioupata kutoka kwa mshambuliaji wa Simba, Okwi na kufunga bao la umbali wa mita 25 katika dakika ya 29 baada ya kumsoma kipa wa Platinum na kugundua kuwa alikuwa amesogea mbele ya lango. Bao hilo linafanana na lile Okwi aliloifunga Yanga wiki moja iliyopita.
Niyonzima alifunga bao la pili katika dakika ya 42 kwa ribaundi baada ya Mrundi Amissi Tambwe kupiga shuti kali lililookolewa na kipa wa Platinum, Petros Mhari, ingawa wageni walizinduka na kupata bao lao pekee dakika ya 45 kwa mpira wa adhabu uliopigwa na Walter Musoma.
Tambwe dakika ya 46 alipokea pasi ya Ngassa na kuwaliza wageni, beki Juma Abdul aliyesababisha bao la kufutia machozi kwa Wazimbabwe alisahihisha makosa yake katika dakika ya 52 baada ya kumtengenezea Ngassa krosi safi iliyozaa bao la nne kwa Yanga.
Kocha wa Platinum, Norman Mapeza alifanya mabadiliko katika dakika ya 46 na 60 lakini hayakusaidia kwani Yanga walionekana kuwa imara kwa dakika zote 90.
Yanga ililazimika kumtoa beki Juma Abdul aliyeumia katika dakika ya 75 na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga.
Awali Yanga ilimtoa Simon Msuva katika dakika ya 68 na nafasi yake kuchukuliwa na Mliberia, Kpah Sherman.
Ngassa alikamilisha karamu ya mabao kwa Yanga katika dakika ya 90 baada ya kufunga kwa shuti kali kufuatia pasi ya Sherman.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul/Dilunga, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa, Msuva/Sherman.