Injinia atoa changamoto ukarabati Uwanja wa Azam Complex kwa ajili ya Afcon

Muktasari:
- Uwanja wa Azam Complex umekarabatiwa kwa gharama ya Sh 400milioni ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.
Dar es Salaam. Kama ulikuwa unadhani ukarabati wa Uwanja wa Azam Complex ni rahisi basi si utakuwa umepotea, jamaa wamepambana vya kutosha kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa kuendana na matakwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Injinia mkuu wa uwanja huo, Victor Ndozelo alisema wakati wanafanya marekebisho ya uwanja huo wamekutana na changamoto nyingi, lakini wamefanikisha yote.
"Kubadilishwa kwa miundombinu ilikuwa changamoto kubwa, kila anayekuja anakuja na la kwake, lakini lengo kubwa ni kuhakikisha mashindano yaende vizuri," alisema.
Alisema licha ya changamoto zote ambazo amepitia akifanya kazi na CAF amejifunza vitu vingi ambavyo vimemuongezea vitu katika kazi yake.
"Caf wanajali muda, ubunifu na mazingira kuwa bora kwa kila mmoja kulizika nayo, lakini kufanya kazi kwa ushirikiano kwa sababu hata hapa lilikuwa ndio lengo kuu na tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa," alisema Ndozelo.
Aliongeza kupitia maandalizi waliyoyafanya wapo tayari kupokea timu yoyote ambayo itakwenda uwanjani hapo, miundombinu yote ipo vizuri kwa wao kukaa na kuchukua mahitaji yao yote.