Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ilombe Mboyo: Mashabiki West Ham wamkataa kwa sababu ya kubaka kabinti

Ilombe Mboyo

Muktasari:

  • Mboyo akiwa mjini Brussels alijiunga na timu ya vijana ya Anderlecht na baadaye alihamia katika timu ya vijana ya Club Brugge kabla ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka 14 na kufungwa jela wakati huo Mboyo akiwa na miaka 17 na alikuwa ni mwanachama wa kundi la watoto watukutu katika Wilaya ya Matonge mjini Brussels.

BRUSSELS, UBELGIJI

ILOMBE Mboyo alikaribia kusajiliwa na klabu ya West Ham United ya England msimu huu, lakini mashabiki wa klabu hiyo waliposikia kwamba aliwahi kufungwa kwa sababu ya kubaka, walilalamika katika mitandao ya kijamii hivyo uongozi wa West Ham ukaacha kumsajili.

Hapa kuna swali, mchezo wa soka unaweza kumbadilisha mtu mhalifu kuwa mtu mwema?

Hilo limetokea kwa Mboyo kwani alifungwa jela miaka saba baada ya kukubali kosa na kuwajibika kwa kosa hilo huku akiendelea kucheza soka akiwa jela na kutoka akiwa amebadilika kitabia.

Mboyo (27), alizaliwa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini alikulia nchini Ubelgiji katika mitaa ya Brussels na kucheza soka mitaani akiwa na beki wa Manchester City, Vincent Kompany. Mboyo akiwa mjini Brussels alijiunga na timu ya vijana ya Anderlecht na baadaye alihamia katika timu ya vijana ya Club Brugge kabla ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka 14 na kufungwa jela wakati huo Mboyo akiwa na miaka 17 na alikuwa ni mwanachama wa kundi la watoto watukutu katika Wilaya ya Matonge mjini Brussels.

Kitendo hicho cha Mboyo kubaka kilimgharimu kwani alifungwa jela miaka saba. Mtafutaji wa vipaji vya wachezaji (scout), Pierre Bodenghien ndiye aliyegundua kipaji cha Mboyo akiwa jela.

“Ana kila kitu, urefu mzuri, ufundi, mwili uliojengeka vizuri na ana uwezo mzuri wa kutumia miguu yote,” anasema Bodenghien.

Aligunduaje kipaji cha Mboyo?

Bodenghien anasema alikuwa mjini Brussels akaamua kwenda kuangalia mazoezi ya soka ya wafungwa katika jela ya Ittre ambayo yalianzishwa na Malkia wa Ubelgiji, Paola, tangu mwaka 1995 yaliyokuwa yakiitwa ‘Soka Ndani ya Jela’. Kwa kuwa Bodenghien anafanya kazi ya kutafuta vipaji vya wachezaji kwa muda wa miaka 20 alikiona kipaji cha Mboyo na hivyo akawafuata viongozi wa klabu ya Charleroi ya Ubelgiji na kuwashawishi wamsajili.

Pia wakati akiwa jela, Mboyo alionyesha tabia nzuri hivyo ilikuwa ni rahisi kwa klabu ya Charleroi kuushawishi uongozi wa Jela ya Ittre kumruhusu Mboyo kufanya mazoezi na wachezaji wa timu ya Charleroi.

Wakati huo kocha wa Charleroi alikuwa ni kiungo wa zamani wa Scotland, John Collins na anasema: “Mboyo alipokuja alifanya mazoezi kadhaa ya pasi na kumiliki mpira na baada ya hapo nilikuwa nikimjumuisha katika mechi mbalimbali za kirafiki.

“Alikuwa akija kucheza mechi hizo za kirafiki halafu anarudi jela, alikuwa akifanya hivyo mara moja au mbili kwa wiki, tulikuwa tukiongea naye pia kuhusu masuala ya nidhamu, heshima na kufanya kazi kitimu.”

Naye kocha Collins anasema: “Katika kipindi chote hicho, Mboyo alikuwa mkimya na mtulivu tofauti na tulivyokuwa tukimchukulia mtu anayetoka jela, lakini aliweza kutoa ushirikiano wa hali ya juu. “Tabia yake ilikuwa ya hali ya juu, alifanya kazi ya kucheza soka kwa bidii na kushirikiana vizuri na wenzake, niliamini kila mtu anahitaji nafasi ya pili katika maisha.”

Baada ya kumaliza kifungo chake na kuachiwa huru, Mboyo alijiunga rasmi na klabu ya Charleroi mwaka 2009, Mei 2010, Mboyo alijiunga na klabu ya Kortrijk kwa mkopo na klabu hiyo ilimsajili rasmi Septemba 2010 na kuichezea kwa mafanikio kabla ya Januari 2011 kuhamia klabu ya Gent.

Akiwa na klabu ya Gent ndipo nyota yake ilivyozidi kung’ara kwani katika mechi 80 alizoichezea klabu hiyo, ameifungia mabao 37 na kubatizwa jina la ‘Le Petit Pele’ (Pele Mdogo).

Kutokana na uwezo mkubwa wa kutandaza soka aliounyesha, mwaka 2012, Mboyo alipewa unahodha katika klabu ya Gent na Oktoba 2012 aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji.  Akiwa na kikosi cha Ubelgiji mwaka huu, Mboyo amecheza mechi mbili za kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014 akicheza timu moja na nyota Christian Benteke, Marouane Fellaini, Dries Mertens, Eden Hazard na Vincent Kompany.

Ubelgiji sasa ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali hizo za Kombe la Dunia na kama itafuzu, Mboyo anatarajiwa kuwapo na kikosi hicho nchini Brazil.

Hata hivyo kwa jinsi umaarufu wa Mboyo unavyozidi kupanda ndipo watu pia wanaangalia maisha yake ya nyuma na kuona nyota huyu alifungwa jela miaka saba kwa kesi ya kubaka.

Wapo watu wanaoona hafai kabisa kupata umaarufu anaopewa kutokana na kosa alilowahi kulifanya, lakini Mboyo kwa upande wake anasema: “Jambo hilo lilitokea zamani na wakati nikiwa jela niligundua kosa kubwa nililolifanya, nilikubali kuwajibika.”

Nalo Shirikisho la Soka la Ubelgiji linamtetea nyota huyo hadharani, na Rais wa Shirikisho hilo anasema: “Watu wanapomaliza kifungo siyo lazima iwe wamepotea kabisa katika jamii, ni rahisi kuwalaumu watu wanaofungwa, lakini tunaweza kumtumia Mboyo kuwafundisha vijana wajiepushe na vitendo vibaya katika jamii kwa sababu yeye amejifunza mengi na amebadilika kitabia.”

Hata hivyo, mtazamo wa kwamba Mboyo amebadilika kitabia na kuwa mtu mwema haujapokewa na kila mtu kwani msimu huu klabu ya West Ham ilikaribia kumsajili, lakini mashabiki wa timu hiyo walipogundua maisha ya nyuma ya Mboyo, walianzisha kampeni katika mitandao ya kijamii kupinga nyota huyo asisajiliwe hivyo hakusajiliwa.

Mmiliki wa klabu ya West Ham, David Sullivan, anasema: “Sikwenda kinyume na mashabiki wetu, nilitaka maoni yao na wao wakamkataa Mboyo kwa sababu zamani alibaka.”

Mboyo kwa sasa anaendelea kuichezea klabu ya Genk ya Ubelgiji.