Huyu ndiye Juma Mahadhi

Muktasari:
- Aingia na bao lake, Chirwa ni yule yule
JUMA Mahadhi akitokea benchi katika kipindi cha pili cha pambano la awali la Ligi ya Mabingwa Afrika na kuifungia Yanga bao pekee lililowapa ushindi mwembamba mbele ya St Louis ya Shelisheli, huku Obrey Chirwa akikosa tena penalti.
Ushindi huo haukuwapa furaha mashabiki wengi wa Yanga waliofurika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ila kwa upande mwingine ni kama waliamua kuwakomoa watani zao Simba waliohamasishwa kujitokea kuishangilia Yanga.
Siku moja kabla ya pambano hilo, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alikaririwa akiwataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuishangilia Yanga na kama watashindwa basi wakae kimya badala ya kuizomea.
Lakini Yanga ilichofanya ni kama iliwapunguzia mzigo watani wao kwa kumaliza dakika 45 matokeo yakiwa suluhu baada ya Obrey Chirwa kuendeleza tatizo lake la kukosa mikwaju ya penalti baada ya kuinyima Yanga bao la mapema.
Yanga ilipata penalti dakika ya 24 baada ya beki Hassan Kessy kuchezewa rafu ndani ya boksi la timu ya St Louis na beki Rokotoarison na mwamuzi kutoka Ethiopia, Belay Tadesse Asserese aliamuru adhabu hiyo na Chirwa aliuwahi mpira uliokuwa miguuni mwa Ibrahim Ajib na kutaka kuipiga penalti hiyo.
Hata hivyo, kama kawaida yake, Mzambia huyo alipoteza mkwaju huo kwa kupiga pembeni ya lango, ikiwa ni penalti yake ya tatu kupoteza ndani ya mwezi mmoja. Alikosa katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA na kisha kukwama tena Yanga ilipoumana na IHEFUya Mbeya katika mechi ya Kombe la FA.
MASHABIKI WACHUKIA
Soka bovu lililochezwa na Yanga mbele ya St Louis ambao ilitabiriwa labda wangepigwa nyingi kwa kurejea rekodi ilizonazo Yanga dhidi ya timu za Visiwa vya Bahari ya Hindi, liliwakera mashabiki wa klabu hiyo waliofurika uwanjani.
Mara ya mwisho Yanga kuvaana na St Louis jijini Dar es Salaam, iliifumua mabao 4-1 na kuhitimisha safari ya Washelisheli hao katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1992 kwa jumla ya mabao 7-2 kwani katika mchezo wa kwanza waliifunga 3-1 kwao.
Ingawa Yanga ilishinda, lakini mashabiki hawakufurahishwa na jinsi timu yao ilivyocheza hasa kipindi cha kwanza ambapo wageni walifanya mashambulizi kadhaa ya kushtukiza na kumpa kashkash kipa Ramadhan Kabwili, huku wakizuia lango lao kwa ustadi mkubwa na kuwapa ugumu vijana wa George Lwandamina kupenya kusaka mabao.
Licha ya Yanga kufanya mashambulizi kadhaa kupitia Kessy, Tshishimbi aliyeng’ara katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Yanga, dakika 45 ziliisha bila timu yoyote kupata bao.
MAHADHI MTAMU
Kipindi cha pili kilianza kwa mchezo uliopooza bila ya kuwepo kwa mashambulizi ya maana kabla ya dakika ya 60 wageni kumtoa Rakotoarison na kumwingiza Yannick Julie na dakika moja Ajib ambaye hakuwa na makali yaliyozoeleka alipoteza nafasi ya kuipa Yanga uongozi kwa kushindwa kumalizia krosi tamu ya Chirwa aliyewatoka mabeki wa St Louis.
Louis walimtoa tena Hall na kumuingiza Marvin Mathiot dakika ya 62 na dakika nne baadaye Yanga iliwapumzisha kwa mpigo Ajib na Emmanuel Martins
na kuwaingia Juma Mahadhi na Geofrey Mwashiuya walioiongezea Yanga uhai. Mahadhi na Mwashiuya waliifanya Yanga ichangamke mbele na kuwakimbiza wageni na kupata kona dakika moja tu tangu waingie yuwanjani. Kona hiyo ilichongwa na Mwashiuya na kuunganishwa kwa kichwa na Tshishimbi kabla ya kuokolewa na mabeki wa St Louis na ndipo Mahadhi akafanya yake kwa kuutupia kambani akiiandikia Yanga bao hilo pekee.
Bao hilo liliwashtua St Louis na kuanza kushambulia kwa kasi na kuifanya Yanga kufunguka na katika dakika ya 72 Chirwa alishindwa kukwamisha mpira wavuni kwa kupaisha mpira aliomegewa krosi na Mwashiuya aliyewatoka mabeki wa wageni.
Dakika ya 86 Yanga ilimtoa Pius Buswita aliyekosa mabao mengi ya wazi katika mchezo huo wa jana na nafasi yake kuchukuliwa na Yusuf Mhilu kabla ya dakika
moja baadaye wageni kumtoa Gervas na kumuingiza Roddy Melanie.
KAZI WANAYO
Hadi dakika 90 zilipomalizika, Yanga ilitoka uwanjani na ushindi huo kiduchu na kuwapa kazi kwa mchezo wao wa marudiano utakaopigwa Februari 20 kwani itahitajika kushinda ama kupata sare yoyote ili kusonga mbele.
Kama itaing’oa St Louis, Yanga itakuwa na kazi ya kuvaana ama na Township Rollers ya Botswana iliypata ushindi wa kishindo nyumbani dhidi ya El Merreikh ya Sudan waliofumuliwa mabao 3-0 mjini Gaborone.
Mshindi wa mechi hiyo ya Watswana na Wasudan ndiye atakayecheza na Yanga ama St Louis katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo kusaka tiketi ya
kutinga makundi.
NSAJIGWA ANENA
Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema kipindi cha kwanza walipata ugumu kutokana na wageni kushindwa kufunguka, tofauti na kipindi cha pili walipojipambanua baada ya kufungwa bao na Mahadhi.
“Ni timu nzuri na tuna kazi katika mechi ya marudiano, St Louis sio wabaya kwani tuliwatambua baada ya kuwafunga. Pia kukosa mabao mawili ya wazi ikiwamo penalti imetuweka kwenye mtihani, ila tutaenda kupambana ugenini,” alisema.
Naye mfungaji wa bao pekee la Yanga, Mahadhi alisema anashukuru kuipa Yanga ushindi huo, japo alikiri mechi ilikuwa ngumu tofauti na walivyotarajia.