Hiyo spidi ya Simba balaa

KAMA Simba watatua kwenye mashindano na spidi wanayoonyesha mazoezini, kuna timu zitapata tabu.
Simba imeweka kambi mjini hapa kujiweka sawa tayari kwa Simba Day, michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara huku ikionyesha morali ya aina yake kiasi cha kushindwa kutofautisha mchezaji mgeni na wa zamani.
Mwanaspoti lilishuhudia awamu mbili za mazoezi ya asubuhi na jioni. Katika programu ya asubuhi Kocha Didier Gomes na timu ya ufundi walikuwa wakiwafanyisha wachezaji mazoezi ya mwili na fiziki zaidi na hakukuwa na mpira wowote.
Lakini, jioni wakaanza kuuchezea mpira kwa mbinu mbalimbali huku akiwasisitizia kucheza mpira wa kasi ambao walimudu vizuri zoezi hilo ambalo amekuwa akiliwekea mkazo tangu timu itue mjini hapa.
Gomes amewakosha viongozi wa Simba waliopo hapa ambao mazoezini wanaonekana kufurahishwa zaidi na spidi ya timu haswa kutokea pembeni, mfumo ambao umeifanya kuwa na kasi zaidi ya ile ya misimu miwili iliyopita. Mastaa kama Pape Sakho, Yusuph Mhilu na Peter Banda ni miongoni mwa wachezaji wapya ambao jana waling’ara kwenye mazoezi ya jioni na kuwafanya viongozi kutikisa vichwa kwa furaha.
Wachezaji waliokuwa kwenye timu za taifa Tshabalala, Nyoni, Banda, Muzamiru na Kapombe jana walikuwa wakifanya mazoezi ya pekee yao ili kuchanganya kwanza kuendana na kasi ya wenzao walioiva zaidi.