HISIA ZANGU: Sh 80 Milioni za Mwamnyeto zinazua maswali
COASTAL Union wanaleta mambo ya Ulaya. Wametangaza kutaka dau la Sh80 milioni kwa klabu kubwa zinazomtaka mlinzi wao wa kati, Bakari Nondo Mwamunyeto. Ni pesa nyingi katika soka. Jeuri hiyo wameipata wapi? Hatujui sana.
Kuna sehemu wameipata jeuri hiyo. Labda jinsi beki wao alivyojihakikishia nafasi katika kikosi cha Taifa Stars huku akitokea katika klabu ambayo ipo nje ya Azam, Simba na Yanga. Haya mambo yalitokea zamani.
Lakini inawezekana wamepima kiwango cha beki wao huyu mahiri kisha wakagundua kuwa ni bora sana halafu kule kwengineko kwa wakubwa kuna mabeki ambao umri umeanza kuwapita. Akina Kevin Yondani, Erasto Nyoni na Paschal Wawa.
Lakini inawezekana wameona wameshikilia dhahabu mkononi na labda klabu kubwa huenda zikapata uvivu wa kwenda nje ya mipaka kusaka walinzi wa kigeni na badala yake chaguo lao la kwanza likawa kwenda Tanga kumpata mlinzi huyu.
Nje ya hoja hizo kuna maswali yanaibuka kuhusu dau ambalo Coastal wametangaza kwa beki kwao. Swali la kwanza. Je kuna mchezaji mwenye thamani ya Sh80 milioni hapa nchini? Mpaka sasa hakuna mchezaji aliyewahi kununuliwa kwa dau hilo.
Mchezaji ghali mpaka sasa anabakia kuwa Mrisho Ngassa ambaye Yanga walimuuza kwenda Azam miaka kadhaa iliyopita kwa dau la Sh50 milioni katika utawala wa Mwenyekiti wa zamani, Iman Madega.
Hapa tunazungumzia dau ambalo klabu fulani inapata kwa kumuuza mchezaji mwenye mkataba. Hatuzungumzii kiasi ambacho mchezaji atalipwa mwenyewe mkononi pindi akishauzwa. Anko Ngassa anabakia kuwa mchezaji wa mwisho kuuzwa ghali.
Kwa kiasi kikubwa inawezekana Coastal Union wameona kuna baadhi ya wachezaji waliletwa nchini kutoka kwa gharama ya zaidi Sh100 milioni, lakini hawafikii ubora wa Mwamnyeto. Simba, Yanga na Azam wakati zinapokumbana na bei hii nadhani na hili walifikirie pia. Tuanze kuthamini bidhaa za nyumbani.
Mtaani kuna minong’ono kwamba “huyo beki hana thamani hiyo” wengine wanasemena “hawa Coastal waache tamaa”. Lakini hii yote ni kwamba kwa sababu wanamjua Mwamnyeto. Wamemuona tangu akikua. Wanakutana naye mitaani. Wakati mwingine kujuana ni shida.
Kama Mwamnyeto angekuwa ni beki kutoka AS Vita au Al Masri si ajabu tusingehoji sana kuhusu dau hilo. Tatizo linaanzia pale kwamba ni Msambaa tu wa Tanga. Amekulia mitaani humu humu na tunamjua tangu akiwa mtoto.
Ukifikiria bei za baadhi ya wachezaji wa kigeni walioletwa hapa nchini na wala hawakuwa na msaada mkubwa na klabu zao unagundua kwamba hakuna ajabu sana kwa Mwamnyeto kuuzwa bei hiyo. Labda tu kwa sababu tuna kasumba sana ya kupenda wachezaji wa kigeni.
Lakini hapo hapo inafikirisha zaidi. Siku hizi wachezaji wa nafasi ya ulinzi Tanzania wanaonekana kuwa adimu kuliko washambuliaji. Walinzi wanaonekana kuwa na thamani zaidi. Hivi tukiwaweka sokoni washambuliaji wazawa pamoja na walinzi nani ana thamani kubwa?
Inawezekana Mwamnyeto akawa ghali kuliko washambuliaji wetu. Inawezekana Shomari Kapombe au Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wakawa na thamani kuliko washambuliaji wetu. Washambuliaji wetu wa kileo wana matatizo ya msingi.
Pale England mchezaji ghali ni mlinzi, Harry Maguire lakini ni wazi kwamba kuna wachezaji wenye thamani zaidi kuliko yeye. Harry Kane, Raheem Sterling, Marcus Rashford wana thamani zaidi ni vile tu yeye Maguire alipata nafasi ya kuuzwa.
Kitu kingine cha msingi zaidi kuhusu Mwamnyeto ni kwamba huenda viongozi wetu wanaona ugumu wa kutoa dau hilo kwa sababu wanataka wakimnunua mchezaji awe amefika klabuni. Ukweli ni kwamba kwa mchezaji kama Mwamnyeto unaweza kumnunua na kumuuza baadaye.
Klabu lazima ziwe zinawanunua wachezaji kwa lengo la kuwauza pia siku za usoni. Sisi tunaona ugumu kwa kununua kwa sababu hatuna mipango ya kuwauza wachezaji kwa siku za usoni (resale value). Mchezaji kama Mwamnyeto anaweza kuuzwa ndani ya miaka miwili kwa dau la dola 100,000 na zaidi kama akicheza katika michuano mikubwa. Hili ni kadirio la chini zaidi. Mara nyingi wachezaji hawapo katika thamani halisi. Dunia ya leo ya kibiashara imewapandisha wachezaji bei. Moja kati ya sababu ya kuwapandisha bei ni ukweli kwamba klabu zinazowanunua zinaweza kuwauza.
Suala hili hili la Mwamnyeto, kiongozi mmoja wa timu kubwa aliwahi kuniambia kwamba kwa vile mchezaji huyu amebakiza mkataba wa mwaka mmoja pale Tanga basi wanaweza kumuacha ili wamchukue bure mwishoni mwa msimu. Hivi tutanyemelea wachezaji wa bure mpaka lini?
Kwa muda mrefu sasa klabu ndogo zimekuwa hazinufaiki na zinakandamizwa zaidi kwa sababu wachezaji wake wamekuwa wakiondoka bure. Klabu kubwa zimegoma kuwaongezea uwezo wa kipesa klabu ndogo kwa sababu bado zinachukua wachezaji mahiri wa timu ndogo bure.
Kama Coastal wakifanikiwa kumuuza Mwamnyeto walau kwa dau la Sh50 milioni basi wanaweza kuzitumia pesa hiyo vyema kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao. Walau wanaweza kuunza msimu ujao wakiwa na nguvu ya kipesa.
Sina nia ya kutetea sana dau la Mwamnyeto lakini nadhani wakati umefika sasa tupigie debe biashara ya mauzo ya wachezaji kuliko habari za kunasa wachezaji walio huru. Tunahitaji biashara katika soka. Tusiwe watu wa maneno mengi kuhusu soka la Ulaya lakini linapofika suala la soka letu tunakimbia biashara zenyewe.